Mojtaba Khamenei ateuliwa kiongozi mkuu wa Iran

Babake Ali Khamenei aliuawa kwenye mashambulizi yaliyotekelezwa na Israel na Marekani.

Marion Bosire
1 Min Read

Mojtaba Khamenei mwana wa marehemu kiongozi mkuu wa Iran Ayatolla Ali Khamenei ameteuliwa kuwa kiongozi mkuu wa Iran kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na babake.

Tayari viongozi wa kijeshi na wale wa kisiasa wameapa kuwa watiifu kwa kiongozi mpya Mojtaba Khamenei wa miaka 56.

Haya yanajiri wakati ambapo Marekani kwa ushirikiano na Israel zinaendelea kushambulia Iran ambapo milipuko imeripotiwa katika maeneo ya Qom na Tehran.

Hatua hii inafuatia pia mashambulizi yaliyotekelezwa na Israel dhidi ya vituo muhimu vya mafuta vya Iran hali iliyosababisha moshi mkubwa juu ya jiji kuu la Iran.

Seneta Lindsey Graham wa Marekani anaonekana kughadhabishwa na uteuzi wa Motjaba kuwa kiongozi mkuu wa Iran akidai kwamba yeye sio mabadiliko ambayo Marekani inatafuta.

“Ninaamini kwamba itagharimu muda mfupi tu kabla akutane na yaliyomfika babake.” Alisema Graham kwenye chapisho lake la mtandao wa X.

Graham amekuwa akihimiza mashambulizi dhidi ya Iran na jarida la Wall Street liliripoti wiki iliyopita kwamba alikuwa amemwelekeza Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kuhusu jinsi ya kutafuta uungwaji mkono wa Rais Trump.

Wanajeshi kadhaa wa Marekani wanaripotiwa kuuawa katika makabiliano nchini Iran, siku moja baada ya Rais Trump kuwatambua walioaga awali katika mzozo huo huo.

Share This Article