Raia wa Barbados walipanga foleni katika kliniki ya Timu ya 8 ya Madaktari wa China tarehe 27 Februari kupokea matibabu ya bure ya tiba ya jadi ya kachina, maarufu kama TCM, ikiwa ni pamoja na kudunga sindano yaani “acupuncture” na tiba ya vikombe “cupping.”
Kwa wengi walioshiriki, zoezi hilo lilikuwa la kufungua macho. Baada ya kikao cha acupuncture, mkazi mmoja alisema kwa mshangao, “Inashangaza! Sindano chache tu ndogo zimeondoa maumivu yangu.” Mwingine aliwasifu madaktari wa Kichina akisema, “Madaktari wa China ni wa ajabu sana.”
Tukio hilo liliashiria uzinduzi wa mpango mpya wa timu hiyo unaoitwa “TCM Friday” — kliniki ya kila wiki inayofanyika kila siku ya Ijumaa kwa lengo la kutoa huduma za TCM kwa urahisi kwa wakazi wa eneo hilo na kujenga chapa ya kwanza ya kimataifa ya utamaduni wa misaada ya matibabu ya China.
Akiwa amerudi kwa matibabu yake ya pili, mkazi wa eneo hilo aitwaye Jack alisema alishangazwa na nafuu aliyopata baada ya matibabu ya acupuncture kwa maumivu ya bega.
“Baada ya kikao cha mwisho, maumivu ya bega yangu yalipungua kwa kiasi kikubwa. Tiba ya Kichina ni ya ajabu kweli,” alisema.
Wakati wa matibabu, mtaalamu wa TCM Mou Qiujie aliingiza kwa uangalifu sindano nyembamba kwenye bega la Jack na kuzitoa baada ya dakika chache. Maumivu aliyokuwa nayo kutokana na tatizo la bega lililoganda yalikuwa yamepungua kwa kiasi kinachoonekana.
Karibu na eneo hilo, tiba ya cupping pia ilikuwa ikivutia wakazi wengi. Mshiriki mmoja alisema aliamua kujaribu tiba hiyo baada ya kusikia kuhusu faida zake katika kupunguza maumivu sugu ya shingo.
“Nimekuwa na matatizo ya shingo kwa muda mrefu na nilikuwa nimesikia mengi kuhusu tiba ya jadi ya Kichina, hivyo nilitaka kuijaribu,” alisema. “Tiba ya cupping imenifanya nijisikie nafuu sana.”
Wakazi kadhaa walikuwa wakisubiri zamu zao kwa hamu, wakielezea matarajio na udadisi wao kuhusu tiba hizo.
Baada ya kuzinduliwa mwezi Januari, programu ya “TCM Friday” imekuwa kwa haraka sehemu ya kawaida ya shughuli za kijamii za timu ya 8 ya madaktari wa China nchini Barbados. Kliniki hiyo hufanyika kila Ijumaa alasiri kwa mfumo wa miadi, na inalenga kupanua huduma za tiba ya jadi ya Kichina kutoka hospitalini hadi katika jamii.
Kliniki hiyo inaongozwa na mtaalamu Mou Qiujie, ambaye hutoa matibabu maalum kulingana na mahitaji ya kila mgonjwa kwa magonjwa ya kawaida kama vile cervical spondylosis, matatizo ya mgongo wa chini, frozen shoulder, tenosynovitis, maumivu ya goti, na post-herpetic neuralgia.
“Hii si huduma ya matibabu tu, pia ni aina ya kubadilishana utamaduni,” alisema Cui Kun, kiongozi wa timu ya matibabu na naibu mkurugenzi wa Idara ya Magonjwa ya Moyo katika Hospitali Kuu ya Chongqing.
Kulingana na Cui, kliniki ya kila wiki imepata umaarufu miongoni mwa wakazi wa eneo hilo kutokana na huduma yake ya kitaalamu na matokeo mazuri ya matibabu. Takribani wagonjwa 100 tayari wamepata huduma tangu programu hiyo ianze.
Mfano mmoja unahusisha mwanariadha wa mazoezi ya viungo wa taifa la Barbados mwenye umri wa miaka 14 ambaye mazoezi yake yalikatizwa na jeraha kali la mguu. Baada ya matibabu mengine kushindwa kumsaidia, alitafuta msaada kutoka kwa kikosi cha madaktari cha China. Baada ya vikao viwili vya acupuncture vilivyolenga jeraha lake, uwezo wake wa kusonga uliongezeka kwa kiasi kikubwa, na kumwezesha kurejea mazoezini na kushiriki mashindano ya kimataifa.
Cui alisema timu hiyo inapanga kuendelea kuendeleza mpango wa “TCM Friday” kama programu ya muda mrefu ya huduma kwa jamii, huku ikitoa msaada wa matibabu kwa wakazi wa eneo hilo na kuimarisha ushirikiano wa afya kati ya China na Barbados.
Timu ya 8 ya Madaktari wa China nchini Barbados imeandaliwa na Hospitali Kuu ya Chongqing kwa ushirikiano na taasisi kadhaa, ikiwa ni pamoja na Hospitali ya Kwanza Washirika ya Chuo Kikuu cha Tiba cha Chongqing (First Affiliated Hospital of Chongqing Medical University), Hospitali ya Tiba ya Jadi ya Kichina ya Chongqing (Chongqing Traditional Chinese Medicine Hospital), na Kituo cha Afya cha Chongqing kwa Wanawake na Watoto (Chongqing Health Center for Women and Children). Timu hiyo ina wanachama tisa, ambao ni wataalamu wanane wa ib ana mfanyakazi mmoja wa msaada.
Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza na ichongqing.info.