Timu ya wanawake ya Kenya Harambee Starlets ilishindwa goli moja bila jibu na wenyeji Ivory Coast katika pambano la kirafiki Jumatano usiku.
Mechi hiyo ilisakatwa katika uwanja wa Allasane Quattara mjini Abidjan.
Starlets wanaojiandaa kushiriki kipute cha mataifa ya Afrika (WAFCON) kuanzia wiki ijayo, wamekuwa na wakati mgumu katika maandalizi baada ya kupigwa tena magoli 2-0 na Benin katika mechi ya kwanza ya kujipima nguvu mapema wiki hii.
Kenya inatarajiwa kufunga safari leo kuelekea Marseille, Ufaransa kwa kambi ya mazoezi kabla ya kutua Morocco Machi 15 kwa dimba la WAFCON.
Starlets wako kundi A pamoja na Algeria, Senegal na wenyeji Morocco wanaposhiriki WAFCON kwa mara ya pili.