Achani azindua ujenzi wa ukumbi wa kijamii

Tom Mathinji
1 Min Read
Gavana wa Kwale Fatuma Achani azindua ujenzi wa ukumbi wa mikutano.

Gavana wa Kaunti ya Kwale Fatuma Achani amezindua rasmi ujenzi wa ukumbi wa kijamii wa Kinondo, katika eneo la Kigaleni wadi ya Kinondo, kaunti ndogo ya Msambweni.

Ujenzi wa ukumbi huo unalenga kuwapa wenyeji wa eneo hilo sehemu ya hadhi yakufanyia shughli mbalimbali za kijamii ikiwemo mikutano, hafla za kuwawezesha vijana, sherehe za harusi pamoja na warsha za kutoa mafunzo.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi huo, Gavana Achani alisema serikali yake imeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha wakaazi wa kaunti hiyo wanapata fursa ya kuandaa mikutano na kushiriki kikamilifu katika masuala ya maendeleo kupitia ushirikishwaji wa wananchi nyanjani.

Aidha Gavana huyo alidokeza kuwa ujenzi wa ukumbi huo ni sehemu ya juhudi za serikali ya kaunti kuimarisha miundombinu ya kijamii na kukuza mshikamano miongoni mwa wakazi.

Kufikia sasa Kaunti ya Kwale imejenga majumba ya mikutano 30 kwenye wadi zote 20 ndani ya kaunti hio.

Share This Article