Sasa ni rasmi kwamba Tume ya Utumishi wa Umma, PSC ina mwenyekiti mpya.
Francis Meja alikula kiapo cha utenda kazi wakati wa hafla iliyoongozwa na Jaji Mkuu Martha Koome leo Jumatano.
Jaji Koome amemtaka Meja na timu yake kulitumikia taifa kwa uadilifu mkubwa akisisitiza umuhimu wa tume hiyo kwa taifa.
“Tume ina wajibu mkubwa wa kuhakikisha kuwepo kwa maadili ya kikatiba katika utumishi wa umma, kuimarisha utendaji kazi wa taasisi, na kuendeleza uanataaluma,” alisema Jaji Koome.
“Utumishi wetu wa umma unapaswa kuwa mwajiri bora anayeweka viwango vya ustahiki, uwazi, haki na uadilifu katika uhusianio kati ya mwajiri na mwajiriwa.”
Meja anajaza pengo lililoachwa na Balozi Anthony Muchiri aliyeteuliwa kuwa Balozi wa Kenya nchini Uturuki.