Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Renson Ingonga ameidhinisha kushtakiwa kwa kiongozi wa mashtaka wa mahakama ya Makadara kwa madai ya ufisadi.
Taarifa kutoka kwa afisi ya Mkurugenzi huyo imesema kuwa baada ya kuchunguza kwa kina pendekezo la Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma alibainisha kuwa kuna ushahidi wa kutosha kumfungulia mashtaka Samuel Mugo Kiarie aliyepatikana na makosa ya kupokea hongo kinyume cha sehemu ya 6(1) ya katiba.
“Mshukiwa huyo anapaswa kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya kupokea rushwa,” Ingonga alisema kwenye taarifa.
Aidha, alionya kuwa hakuna mtu yeyote bila kujali cheo au wadhifa wake yuko juu ya sheria na kwamba afisi yake haitasita kumchukulia hatua za kisheria afisa yeyote ambaye atakiuka maadili.
“Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma inajizatiti kutekeleza wajibu wake wa kikatiba kwa kuzingatia sheria,” iliongeza taarifa hiyo.