Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki leo Jumatano amewaongoza viongozi wengine katika kuhudhuria ibada ya wafu ya waathiriwa wa ajali ya ndege iliyotokea eneo la Mosop, kaunti ya Nandi Jumamosi iliyopita.
Ajali hiyo ilisababisha vifo vya watu sita akiwemo mbunge wa Emurua Dikirr Johana Ng’eno.
Maspika Moses Wetang’ula wa Bunge la Taifa na Amason Kingi wa Seneti ni miongoni mwa viongozi wengine wengi wanaohudhuria ibada hiyo inayofanyika katika kanisa la AGC mtaani Karen.
“Daima utakuwa sehemu ya maisha yangu,” alisema mjane Nayianoi Ntutu Ng’eno aliyemwomboleza mumewe wakati akivuta kumbukizi za nyakati nzuri walizokuwa nazo pamoja katika safari yao ya ndoa.
“Ni wakati wa kuhuzunisha, lakini tunashukuru kwamba tuko hapa kusherehekea maisha ya N’eno. Tunathamini urithi anaoacha na tunasherehekea maisha aliyoishi,” alisema kakaka marehemu Ng’eno, Barnabas Ng’eno, kwenye risala yake ya rambirambi.
Familia za watu wengine watano waliofariki kwenye ajali hiyo, akiwemo rubani wa ndege hiyo, George Were, nazo zilisumulia machungu yalizozisibu punde zilipopokea taarifa za kuondokewa na wapendwa wao.
Mazishi ya marehemu Johana Ng’eno yamepangwa kufanyika Ijumaa wiki hii katika kaunti ya Narok.
Viongozi mbalimbali wanaohudhuria ibada hiyo wanaendelea kutoa hotuba zao na tutakuletea taarifa ya kina kuhusu ibaada hiyo katika taarifa zetu zijazo.