Wetang’ula atoa wito wa sheria kali za usalama wa usafiri wa anga

Spika huyo wa Bunge la Taifa ametoa wito huo kufuatia kifo cha watu sita Jumamosi iliyopita, akiwemo mbunge wa Emurua Dikirr Johana Ng'eno.

radiotaifa
2 Min Read
Spika Moses Wetang'ula akiwa na viongozi wengine nyumbani kwa marehemu Ng'eno mtaani Karen

Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula ametoa wito wa kuwekwa sheria kali za usalama wa usafiri wa anga na uangalifu mkubwa wa hali ya hewa kabla ya kusafiri.

Wito wake unakuja siku nne baada ya kufariki kwa mbunge wa Emurua Dikirr Johana Ngéno na watu wengine watano katika ajali ya helikopta katika eneo la Mosop, kaunti ya Nandi.

Akizungumza kufuatia mkasa huo, Wetang’ula alitoa wito kwa wanachama na watumiaji wakiwemo marubaini kuchukua tahadhari zaidi na kutii sheria za usafiri wa anga kama vile kuzingatia hali ya hewa.

“Unahitaji kuzingatia hali ya hewa wakati huu. Tunahitaji kupunguza matumizi ya helikopta,” alionya Spika Wetang’ula.

Alifichua kuwa yeye na ujumbe wake walitumia helikpota hiyo iliyoanguka wiki mbili zilizopita wakati akielezea kutotabirika na hatari zinazohusiana na usafiri wa anga, hasa hali za hewa zisizokuwa thabiti.

Aidha, alitoa wito kwa wabunge kufanyia mapitio kwa dharura sheria zinazosimamia huduma za usafiri wa anga ili kuboresha viwango vya usalama na kupunguza ajali.

“Katika sehemu zingine za dunia, hakuna helikopta inaweza kupaa hadi iruhusiwe na mamlaka ya usafiri wa anga. Tunapaswa kuboresha mpangokazi uliopo na kuwa na sheria kali zaidi,” aliongeza Wetang’ula.

Aliyasema hayo alipowaongoza wanachama wa Tume ya Huduma za Bunge na wabunge kuzuru nyumbani kwa marehemu Ng’eno mtaani Karen kuiomboleza familia ya marehemu inayojumuisha mjane wa mwendazake, Nayianoi Ntutu.

Spika akitumia fursa hiyo kumlimlimbikizia sifa mbunge huyo aliyefariki wakati akitumikia muhula wake wa tatu hadi wakati akipatwa na mauko kwa kumtaja kuwa mtumishi wa umma aliyechapa kazi kwa kujitolea.

“Hili ni tukio baya. Bunge limempoteza mmoja wa viongozi wake bora,” alisema Wetang’ula.

Jana Jumatatu, Rais William Ruto aliwaongoza viongozi wengine kuifariji familia ya marehemu mtaani Karen.

Ibada ya wafu ya marehemu Ng’eno itaandaliwa kesho Jumatano katika kanisa la AGC Karen jijini Nairobi.

Mazishi ya Ng’eno yamepangwa kufanyika Ijumaa wiki hii katika kaunti ya Narok.

Taarifa ya Martin Mwanje na SPU

Share This Article