Wakenya wahakikishiwa uwepo wa mafuta ya kutosha

Serikali imesema imeagiza mafuta yatakayowasilishwa hadi mwisho wa mwezi Aprili mwaka huu na hivyo kuna usalama wa upatikanaji wa mafuta.

Marion Bosire
2 Min Read
Opiyo Wandayi, Waziri wa Nishati

Waziri wa Nishati Opiyo Wandayi amewahakikishia Wakenya kwamba Kenya ina hifadhi ya kutosha ya mafuta na hivyo kuwaondolea wasiwasi kutokana na yanayoendelea katika Mashariki ya Kati.

Katika taarifa, Wandayi alielezea kwamba mafuta yanayotumika humu nchini huagizwa kutoka eneo la Mashariki ya Kati linalokumbwa na mzozo.

“Kwa kuzingatia yanayoendelea Mashariki ya Kati ambapo huwa tunatoa bidhaa za petroli, Wizara imetathmini hali ya hifadhi ya mafuta,” alisema Wandayi katika taarifa hiyo akiongeza kwamba Kenya ina mafuta ya kutosha kwa matumizi yake na hata kwa kanda.

Waziri Wandayi alisema tayari wameagiza mafuta yatakayowasilishwa hadi mwisho wa mwezi Aprili mwaka huu na hivyo kuna usalama wa upatikanaji wa mafuta.

Wakati huo huo, Wandayi amesema Wizara ya Nishati  inafuatilia hali katika eneo la Mashariki ya Kati ikishauriana na wawasilishaji wa mafuta hayo ili kuweka mikakati.

“Tungependa kuhakikishia umma na wadau wote kwamba Wizara inasalia macho na itaendelea kuchukua hatua faafu kuhakikisha upatikanaji endelevu wa mafuta,” alimalizia Wandayi.

Marekani kwa ushirikiano na Israel ilishambulia Iran Jumamosi, Februari 28, 2026, na kusababisha kifo cha kiongozi mkuu wa taifa Ayatollah Ali Khamenei.

Iran nayo ililipiza kisasi kwa kushambulia vituo vya kijeshi vya Marekani katika mataifa jirani, hali iliyosababisha suitafahamu.

Hali hiyo inakisiwa kutatiza usafirishaji wa mafuta yanayoagizwa kutoka Mashariki ya Kati hadi sehemu mbalimbali ulimwenguni.

Share This Article