Taarifa ya Bruno Mutunga
Baadhi ya wakazi wa maeneo ya Archers Post na Losesia katika wadi ya Waso, kaunti ya Samburu, wamelalamikia kupunguzwa kwa shughuli za British Army Training Unit Kenya (BATUK), wakisema hatua hiyo imeathiri vibaya uchumi wa eneo hilo.
Wakizungumza wakati wa maandamano ya amani katika mji wa Archers Post, wakazi hao walisema kupungua kwa shughuli za jeshi la Uingereza, hasa katika Ranchi ya Kikundi ya Losesia, kumesababisha mamia ya vijana kupoteza ajira na hivyo kuzidisha mateso kwa familia nyingi.
Wakiongozwa na kiongozi wa vijana Moses Lenakio, wakazi hao walisema vijana wengi wamejikuta wakijihusisha na uhalifu na matumizi ya dawa za kulevya kutokana na msongo wa mawazo unaotokana na kupoteza kipato, pamoja na hali ngumu ya kiuchumi inayochangiwa na ukame wa muda mrefu katika kaunti hiyo kame.
BATUK imekuwa ikitoa ajira kwa jamii ya eneo hilo katika kazi za kitaalamu na zisizo za kitaalamu kama vile udereva, ufundi magari, ufundi wa mabomba, umeme, walinzi wa maeneo ya mazoezi ya kijeshi wanaohakikisha usalama wakati wa mafunzo, pamoja na wafanyakazi wa sekta ya ukarimu na wasaidizi wa ofisini.
Wakazi hao waliwalaumu viongozi wa Ranchi ya Kikundi ya Losesia kwa madai ya usimamizi mbovu na kuwatenga wanajamii katika maamuzi muhimu yanayowahusu, ikiwemo uamuzi wa kupunguza shughuli za BATUK katika eneo hilo kubwa ambalo limekuwa likitumika kwa mazoezi ya moja kwa moja kwa miongo kadhaa.
Mwanaharakati wa haki za binadamu, David Lokia, alitaka kufanyika mara moja kwa uchaguzi wa kuchagua viongozi wapya wa Ranchi ya Kikundi ya Losesia, akidai kuwa viongozi wa sasa wamekaa madarakani kwa muda mrefu kupita kiasi na wamefanya maamuzi yanayokwenda kinyume cha maslahi ya wanajamii waliowachagua.
Naye Felix Lekidor aliwashutumu viongozi wa eneo hilo kwa kushindwa kulinda maslahi ya jamii, akiiomba Idara ya Ardhi ya kaunti ya Samburu kuandaa uchaguzi wa viongozi wapya watakaohakikisha kunakuwepo ushirikishwaji wa umma wa kutosha kabla ya maamuzi muhimu yanayowaathiri kufanywa.