Taarifa ya BBC
Watu wapatao 169 wameuawa nchini Sudan Kusini kwenye mashambulizi yaliyotekelezwa juzi Jumapili alfajiri.
Maafisa wa Sudan Kusini wamesema kundi la watu wasiojulikana, lilishambulia walipoanzisha eneo moja kaskazini mwa nchi hiyo.
Waziri wa Habari wa Eneo la Utawala la Ruweng, James Monyluak Mijok, alidai kwamba wavamizi hao walitoka katika jimbo jirani la Unity, na walikuwa na uhusiano na Jeshi la Ukombozi wa Watu wa Sudan katika Upinzani (SPLA-IO).
Hata hivyo SPLA-IO imekana kuhusika katika shambulizi hilo, likishutumu mamlaka ya jimbo la Unity kwa kuingilia vurugu hizo kisiasa.
Umoja wa Mataifa umeonya mara kwa mara kwamba nchi hiyo iko katika hatari ya kurudi kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe.
“Waliokufa ni pamoja na watoto 90, wanawake na wazee, pamoja na maafisa 79 wa vikosi vya kikanda, wakiwemo polisi,” Mijok alisema.
Washambuliaji hao walichoma moto nyumba na masoko wakati wa mapigano yaliyodumu kati ya saa tatu hadi nne.