Mwanamuziki nguli wa Uganda Joseph Mayanja maarufu kama Jose Chameleone amefichua kwamba wakati mmoja aliwaza kuhusu kuhamia nchini Kenya kabisa.
Akizungumza kwenye mahijiano, Chameleone alielezea kwamba wakati huo, wanamuziki tajika walikuwa na ushindani mkubwa na walitawala tasnia ya muziki kabisa kiasi kwamba chipukizi walikosa nafasi.
Alisema studio za kurekodi muziki zilikuwa chache wakati huo, na zilikuwa zikitumiwa na wanamuziki hao muda wote na hawakuwa wanapata fursa za kurekodi muziki.
Jose aliwataja wanamuziki kama Paul Kafeero na Lord Fred Ssebatta, ambao alisema walikuwa walikilipia muda wa studio kwa miezi kama 6 au 8.
Ushindani pia ulifanya iwe vigumu kwake kutumbuiza kwenye maeneo ya burudani ambapo msanii mwenza angempa kipaaza sauti ambacho hakifanyi kazi.
Hali hiyo ilimlazimisha Chameleone kusafiri hadi Nairobi ambapo aliamua kuanza tena kazi ya muziki ambapo alijifunza lugha ya Kiswahili.
Alitagusana na wasanii wa Kenya kama Red San chini ya uongozi wa kampuni ya Ogopa Deejays ambapo walitoa kibao kiitwacho “Bageya” mwaka 1998.
Mwaka 2000 Chameleone alizindua albamu yake ya kwanza kwa jina “Mama Mia” na kutoka hapo akawa anatoa nyimbo nyingi tu.
Kufikia mwaka 2013, Chameleone alikuwa ametoa albamu 13 zikiweno Kipepeo, Shida za dunia, Valu valu, Bayuda, Badilisha, Sweet Banana na Champion.
Nyota yake katika tasnia ya muziki iliendelea kung’aa na hakufika kutekeleza wazo lake la awali la kuhamia nchini Kenya kabisa.