Wizara ya Mambo ya Nje imetoa tahadhari ya dharura kwa Wakenya wanaoishi na wanaozuru nchi za Mashariki ya Kati, ikitaja hali ya usalama inayobadilika na isiyotabirika.
Katika taarifa iliyotolewa Jumamosi na Idara ya Masuala ya ughaibuni, Serikali ya Kenya imewataka raia wake kuwa waangalifu zaidi, ikibainisha kuwa hali inaweza kubadilika wakati wowote bila notisi.
Wakenya walio katika eneo lililoathirika wameshauriwa kujisajili mara moja katika ubalozi au afisi ya ubalozi mdogo wa Kenya iliyo karibu nao.
Watahitajika kusasisha taarifa zao za mawasiliano, taarifa za ndugu wa karibu na mawasiliano ya dharura kupitia jukwaa rasmi la masuala ya ughaibuni.
Raia hao wameshauriwa pia kupunguza safari, kuepuka maeneo ambako operesheni za kiusalama zinaendelea na kuahirisha safari zisizo za lazima, hasa usiku au kipindi cha amri ya kutotoka nje.
Wizara imesisitiza umuhimu wa kufuata kikamilifu maagizo yanayotolewa na serikali za nchi wanazoishi na vyombo vya usalama, huku ikionya dhidi ya kusambaza taarifa ambazo hazijathibitishwa.
Wakenya wamehimizwa kutegemea tu njia rasmi za mawasiliano na kudumisha mawasiliano ya mara kwa mara na familia zao, waajiri na ofisi za kidiplomasia za Kenya.
Walio katika dhiki wameelekezwa kuwasiliana na afisi ya Kenya iliyo karibu au kutumia nambari ya dharura ya ughaibuni inayopatikana saa ishirini na nne.
Katibu wa Masuala ya Ughaibuni Roseline Kathure Njogu amesisitiza tena dhamira ya serikali ya kulinda ustawi wa Wakenya wanaoishi nje ya nchi.