Maafisa wa polisi wamemkamata mshukiwa wa ujambazi, anayeaminika kuwahangaisha wafanyabiashara katika kaunti za Kiambu, Kajiado na Nairobi.
Paul Irungu Mwangi, mshirika wa karibu wa Peter Muhia Njenga, anayedaiwa kuongoza misururu ya wizi wa kimabavu na mauaji katika kaunti za Kiambu, Kajiado na Nairobi, alikamatwa baada ya kukwepa mitego ya maafisa wa usalama kwa siku kadhaa.
Kupitia ukurasa wa X, Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai DCI, ilisema mshukiwa huyo alifumaniwa kwenye maficho yake katika mtaa wa Kasarani, alikokuwa akijificha baada ya washirika wake kutiwa nguvuni wiki iliyopita.
Kulingana na DCI, mshukiwa huyo pamoja na wenzake ambao bado wako mbioni, anahusishwa na genge la utekaji nyara ambalo maafisa wa usalama wanajizatiti kuliangamiza.
Kwa sasa mshukiwa huyo anazuiliwa na maafisa wa polisi, akisubiri kufikishwa mahakamani, huku juhudi zikiendelea za kuwakamata washirika wake.