Mabingwa watetezi Paris Saint-Germain kutoka Ufaransa, wameratibiwa kumenyana na mabingwa wa dunia Chelsea katika raundi ya 16 ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
PSG wataandaa mkumbo wa kwanza Machi 11 ugani Parc De Princes, kabla ya mkumbo wa pili kuandaliwa wiki moja baadaye kiwarani Stamford Bridge.
Kulingana na droo iliyoandaliwa Ijumaa, Galatasaray ya Uturuki itaanzia nyumbani dhidi ya Liverpool tarehe 10 mwezi ujao, Bayern Munich wazuru Italia kumenyana na Atalanta, nao Newcastle United wawaalike Barcelona.
Tottenham Hotspur watakabana koo na Atletico Madrid.
Machi 11 itakuwa zamu ya Arsenal kuzuru Ujerumani kutoana jasho na Bayer Leverkusen, Real Madrid wapimane ubabe na Manchester City, huku limbukeni Bodo Glimt kutoka Norway, wakimaliza udhia dhidi ya Sporting Lisbon.
Washindi watafuzu kwa robo fainali zitakazopigwa kati ya April 7 na 9 na marudio wiki moja baadaye.
Nusu fainali zimepangwa kupigwa kati ya tarehe 28 na 30 mwezi wa nne na marudio juma moja baadaye.
Fainali ya kipute hicho itagaragazwa mjini Budapest, Hungary, Mei 31.