Timu ya taifa ya soka ya wanawake ya Kenya – Harambee Starlets imeratibiwa kucheza mechi mbili za kujipima nguvu kabla ya kushiriki fainali za kombe la mataifa ya Afrika (WAFCON) mwezi ujao nchini Morocco.
Kenya chini ya ukufunzi wa kocha Beldine Odemba, itachuana na Benin tarehe mbili mwezi ujao mjini Abidjan, kabla ya kukabiliana na wenyeji Ivory Coast, Machi nne.
Mechi hizo zitasakatwa katika uwanja wa Allasane Ouattara.
Harambee Starlets itaondoka nchini Jumamosi hii kwa mechi hizo mbili za kirafiki, na baadaye watakita kambi ya mazoezi mjini Miramasa, Ufaransa, hadi Machi 15 watakapoelekea Morocco.
Starlets wamejumuishwa kundi A pamoja na wenyeji Morocco, Senegal na Algeria.
Fainali za WAFCON ambazo Kenya inashiriki kwa mara ya pili zitaandaliwa kati ya Machi 17 na Aprili 3 mwaka huu.