Wakazi wa Isiolo Kusini, wadi zingine 3 wapiga kura uchaguzi mdogo

Uchaguzi mdogo eneo bunge la Isiolo Kusini utafanyika Alhamisi, Februari 26, mwaka huu.

Martin Mwanje
2 Min Read
Vifaa vya uchaguzi mdogo wa Februari 26 vikipokelewa katika uwanja wa JKIA

Wakazi wa Isiolo Kusini leo Alhamisi wanapiga kura kumchagua mbunge wao mpya kwenye uchaguzi mdogo ambao pia unaendeshwa katika wadi zingine tatu nchini.

Wadi hizo ni Muminji and Evuvori katika eneo bunge la Mbeere Kaskazini na Kabras West katika eneo bunge la Malava.

Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa majira ya saa kumi na mbili asubuhi na vinatarajiwa kufungwa majira ya saa kumi na moja jioni.

Wapiga kura ambao watakuwa kwenye foleni wakati wa kufunga vituo wataruhusiwa kupiga kura.

Idadi ndogo ya wapiga walionekana kwenye vituo vya kupiga kura wakiwa tayari kupiga kura.

Hali hiyo imeibua wasiwasi kuwa huenda idadi ndogo ya wapiga kura wakajitokeza kupiga kura kwenye uchaguzi huo mdogo.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imewahakikishia wapiga kura katika maeneo husika kuwa itaendesha uchaguzi huru na wa haki.

Katika eneo bunge la Isiolo Kusini, kinyang’anyiro ni kati ya Tubi Mohamed Tubi wa chama cha UDA dhidi ya dada yake Bina Tubi, anayegombea kiti hicho kupitia tiketi ya chama cha Jubilee.

Kiti hicho kilisalia wazi kufuatia kifo cha baba yao, Mohamed Tubi Bidu, mwezi Novemba mwaka jana.

Mgombea mwingine, aliyekuwa Mwakilishi wa Wadi ya Kinna, Isaack Abduba Fayo, ambaye alikuwa ameidhinishwa na IEBC kugombea kupitia chama cha National Economic Development Party (NEDP) kilichosajiliwa na Gavana wa zamani wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko.

Fayo ambaye alijiondoa katika kinyang’anyiro hicho siku chache zilizopita baada ya kukutana na Rais William Ruto, sasa anaunga mkono mgombea wa UDA.

Share This Article