Wanachama wa ODM wamtaka Oburu ajiuzulu

Marion Bosire
1 Min Read

Baadhi ya wanachama wa kudumu wa Chama cha ODM wamewasilisha ombi wakitaka Oburu Oginga ajiuzulu kutoka nyadhifa zote za uongozi za chama hicho.

Ombi hilo, linaloongozwa na Rachael Tabitha, linaorodhesha madai kadhaa ya Oginga kukiuka taratibu, kama vile uvunjaji wa Kifungu cha 6.2.2(b) cha Katiba ya ODM.

Wanachama husika wanasema ukaidi wa Oburu unadhoofisha misingi ya uwajibikaji, haki na heshima ya taratibu ambazo chamahicho kinawakilisha.

Maamuzi ya Oburu wanasema yamepunguza imani katika miundo ya uongozi ya chama na kuwaacha wanachama wa kudumu wakihisi kutengwa katika maamuzi muhimu ya chama.

Ombi hilo lilisema kuwa vitendo hivi vinaashiria mwelekeo hatari kutoka kwa misingi ambayo ODM imeitetea kwa miongo kadhaa.

Wanachama hao wa kudumu wanataka Oburu Odinga ajiuzulu mara moja, mkutano mkuu wa kitaifa uandaliwe haraka na haki za wanachama wa kudumu zitambuliwe kikamilifu.

Wameipa bodi ya uchaguzi ya kitaifa ya chama hicho siku 30, kutekeleza matakwa yao na  endapo hayatatimizwa, waliotia saini ombi hilo watajiuzulu kutoka ODM kama suala la misingi yao ya maadili.

Share This Article