Maaskofu Tanzania wataka miili ya waliouawa itolewe kwa familia

Marion Bosire
2 Min Read

Baraza la maaskofu wa kanisa katoliki nchini Tanzania, TEC, limeomba kwamba familia zilizopoteza wapendwa wao zipatiwe miili yao kwa ajili ya mazishi.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari, maaskofu hao walisema imethibitika kwamba miili ya baadhi ya waliopoteza maisha, haijapatikana na kwamba inasikitisha ya kuwa baadhi ya watu walipotaka kuwazika wapendwa wao hawakupata miili yao.

Rais wa TEC Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi Mhashamu Wolfgang Pisa akisoma taarifa ya baraza hilo juu ya yaliyotokea siku na baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu alisema kutolewa kwa miili hiyo kwa familia husika kutakuwa jambo la busara.

Askofu huyo wa jimbo la Lindi alisisitiza kwamba ni sharti waliofariki wapumzishwe au kusitiriwa kwa heshima kadri ya imani ya dini, mila, desturi na tamaduni zao.

“Imani yetu inatufundisha kuwa kuna maisha baada ya kifo na kifo ni kuanza maisha mapya na pia miili hii itafufuliwa siku ya mwisho, maana parapanda italia wafu watafufuliwa wasiwe na uharibifu nasi tutabadilika” alisema Askofu huyo.

Haya yanajiri saa chache baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutoa heshima kwa waliofariki wakati wa machafuko yaliyotokea siku ya uchaguzi na ziku kadhaa baadaye.

Alifanya hivyo wakati wa kufunguliwa rasmi kwa bunge la sasa la Tanzania ambapo alitoa pole kwa familia zilizoathirika huku akiagiza kuachiliwa huru kwa waliokamatwa wakati huo na kushtakiwa kwa kosa la uhaini.

Share This Article