Ruto: Mtatumia mfumo mpya wa ununuzi wa kielektroniki, mpende msipende

Kiongozi wa nchi anasema mfumo huo utasaidia kuangamiza ufisadi na pia kuleta uwazi katika kufanya manunuzi serikalini. Mahakama imezuia matumizi ya mfumo huo kufuatia kesi iliyowasilishwa na Magavana.

Martin Mwanje
3 Min Read
Rais William Ruto akiwa na viongozi wengine wakati wa hafla ya kukabilidhi hundi katika Ikulu ya Nairobi Septemba 11

Rais William Ruto amesema serikali kamwe haitarudi nyuma katika kuhakikisha matumizi ya mfumo mpya wa serikali wa ununuzi wa kielektroniki, maarufu kama e-procurement,yanafanikiwa ili kuziba mianya ya ufisadi. 

Aidha, amesema mfumo huo utaleta uwazi katika manunuzi serikalini.

“Tunapoteza hadi asilimia 40 ya fedha za umma kupitia manunuzi. Na hiyo ndio sababu tumesema tunaenda kutumia mfumo wa ununuzi wa kielektroniki ili kila mtu awe na ufahamu. Hakuna haja ya giza. Kama wewe unatuuzia mali kama serikali, shida iko wapi kama wananchi wanajua umetuuzia kwa shilingi ngapi? Kwa nini iwe gizani? Kile tunachosema, ikiwa utaiuzia serikali kitu, wacha ijulikane hadharani. Fulani alituuzia kitu fulani kwa shilingi fulani. Kwa sababu kitu cha shilingi kumi, serikali inanunua na shiling 15 ama shilingi 20. Mbona?,” alishangaa Rais Ruto wakati akiunga mkono matumizi ya mfumo huo.

“Kwa hivyo, tumesema, tuweke kila kitu kwa mtandao hapo. Wewe fulani wa fulani, ulituuzia simiti gunia moja shilingi 2,000. Simiti kawaida kwa duka ni shilingi 700. Haya, maswali sasa tuanze kuulizana kutoka hapo. Ndio mnaona hii kelele yote, mpaka wengine wameenda kortini kuzuia, kwa sababu wanataka kuendelea kuwa hapa kwa giza. Hili giza lazima tuondoe.”

Na kwa wale wanaodhani serikali ina nia ya kuondoa matumizi ya mfumo huo, Ruto alikuwa na ujumbe bayana kwao.

“Ili kuondoa mashaka, wacha niseme, hatutasitisha matumizi ya mfumo wa ununuzi wa kielektroniki kwa sababu tunataka uwazi, na tunataka kuhakikisha Wakenya wanapata thamani ya kodi wanazolipa,”alisema Rais Ruto wakati wa hafla ya kukabidhi hundi iliyofanyika katika Ikulu ya Nairobi siku ya Alhamisi.

Mfumo wa ununizi wa kielektroniki ulipendekezwa na serikali kuu kupitia Wizara ya Fedha. Isitoshe, Waziri wa Fedha John Mbadi ameonya kuwa serikali kuu haitakubali kufanywa kwa manunuzi yoyote nje ya mfumo huo katika hatua inayolenga kuziba husan mianya ya ufisadi na ubadhirifu wa fedha serikalini.

Hata hivyo, Baraza la Magavana (CoG) likiongozwa na mwenyekiti wake Ahmed Abdullahi limetilia dosari mfumo huo likidai utekelezaji wake uliharakishwa na hivyo kutatiza utoaji huduma muhimu kwa raia.

Magavana hao wamesema utekelezaji wa mfumo huo ulifanyika baada ya kufanyiwa majaribio katika kaunti tatu pekee, hatua wanayosema imetatiza mno manunuzi hususan katika sekta ya afya.

Mahakama imesitisha matumizi ya mfumo huo hadi kesi iliyowasilishwa na Magavana hao na watu wengine wanne kupinga matumizi yake itakaposikilizwa na kuamuliwa.

 

Share This Article