Waziri Murkomen awataka wahalifu kusalimisha silaha Elgeyo Marakwet

Martin Mwanje
1 Min Read

Wahalifu wanaomiliki silaha kinyume cha sheria katika kaunti ya Elgeyo Marakwet wametakiwa kuzisalimisha kwa polisi kwa hiari. 

Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen anasema wahalifu hao wako huru kuzisalimisha silaha hizo kwa vituo vya polisi vilivyo karibu nao la sivyo wakione cha mtema kuni.

Kaunti ya Elgeyo Marakwet ni miongoni mwa maeneo yanayokabiliwa na visa vya ukosefu wa usalama wa mara kwa mara, visa ambavyo vimehusishwa na hatua ya wahalifu kumiliki silaha kinyume cha sheria.

“Tunatoa fursa kwa vijana walio na silaha kujisalimisha kwa maafisa wa polisi. Tutawapeleka katika chuo cha kiufundi na kuwapeleka katika maeneo ya ujenzi ili kujenga nyumba za gharama nafuu,” Murkomen aliwahakikishia vijana ambao wako tayari kuitikia wito wake.

“Kuna watu fulani wanaoendesha shughuli zao Marakwet Magharibi na Marakwet Mashariki. Baadhi ni walimu, wengine ni wanakandarasi ambao wananunua bunduki na kusambaza risasi. Jisalimisheni kwa polisi kabla ya mambo kuharibika.”

Waziri Murkomen yuko katika kaunti ya Elgeyo Marakwet kwa mpango wa Jukwaa la Usalama, mpango ambao umemfanya kuzuru kaunti mbalimbali nchini. 

 

Share This Article