Mikutano Miwili, au Lianghui kwa Kichina, ni jina maarufu la vikao mfululizo vya vyombo viwili vikuu vya kisiasa vya China yaani Mkutano wa Baraza la Mashauriano ya Kisiasa la China (CPPCC) na Bunge la Umma la China (NPC).
Mikutano hii miwili ambapo CPPCC ulitangulia kufunguliwa siku ya Jumanne ya tarehe 4 Machi na kufuatiwa na NPC uliofunguliwa rasmi siku ya Jumatano ya tarehe 5 Machi, huwa inafuatiliwa kwa karibu na wawekezaji wa kigeni, huku ikitoa ufahamu muhimu kuhusu hali ya kisiasa ya China, kubainisha vipaumbele vya Beijing kwa mwaka huu mpya, na kuelezea mwelekeo wa jumla wa sera ya nchi.
Mikutano miwili ya China inawakilishwa na watu wa kila hali wakiwemo wanasayansi, wafanya biashara n ahata watu mashuhuri kwenye jamii. Kati ya wajumbe 2,977 wa Bunge la 14 la Umma la China, asilimia 16.69 inawakilishwa na wakulima, asilimia 21.3 inawakilishwa na watalaamu na wasomi, asilimia 14.85 inawakilishwa na makabila madogo, ambapo makabila madogo yote 55 ya China yana wawakilishi wao bungeni. Utaratibu huu wa uwakilishi unahakikisha kwamba maslahi ya watu wa makundi mbalimbali nchini yanaweza kushughulikiwa katika jukwaa la juu zaidi la kisiasa nchini China.
Kwa wale wasiofahamu wanaweza kuona kwamba labda Chama Cha Kikomunisti cha China (CPC) ndio kinatawala katika mchakato mzima wa mikutano hii, hasa katika kufanya maamuzi, la hasha, ukweli ni kwamba kwa kuwa kazi ya kutunga sera ni utaratibu tata, bila shaka watunga sera wanalazimika kusikiliza sauti za makundi tofauti, mikoa tofauti, na pia watu tofauti wenye asili tofauti. Kwa hiyo katika mchakato huu hakika wajumbe wa CPPCC na NPC wana jukumu muhimu, hasa wakati wa mikutano hii miwili.
Kama nilivyosema awali kwamba katika mikutano hii miwili pia vinakuwepo vikao vingine mfululizo vya pembeni vya kamati za chama na serikali za mikoa mbalimbali, pamoja na vikao vya makundi mbalimbali ambavyo mbali na mambo mengine pia hutumika kuwasilisha ripoti zao za kazi. Ripoti hizo hutaja mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita tangu mikutano miwili ifanyike.
Wajumbe wa mikoa mbalimbali ikiwemo Anhui, Ningxia, Qinghai, Shaanxi, Fujian, Zhejiang, Heilongjiang, Jiangsu, Hunan, Guangdong, Xinjiang na Guangxi walifanya vikao vya wazi vinavyoruhusu maswali ya wanahabari, na karibu waandishi wa habari 3000 wa China, wa kanda na nchi nyingine mbalimbali duniani wamehudhuria kwenye Mikutano Miwili na vikao vyake vya pembeni.
Akizungumza na wajumbe wa mkoa wenye nguvu kiuchumi wa Jiangsu, waliokutana tarehe 5 Machi, rais Xi Jinping alisema mkoa wa Jiangsu unapaswa kuongoza katika kuhimiza ushirikiano wa uvumbuzi wa kiteknolojia na viwanda, kuendeleza mageuzi ya kina na kufungua mlango kwa kiwango cha juu, kutekeleza mikakati mikuu ya maendeleo ya taifa na kuwa mfano katika kuleta ustawi kwa watu wote.
Ili kuendeleza uvumbuzi wa kiteknolojia, rais Xi amesema ni muhimu kufanya mfumo wa viwanda kuwa wa kisasa na kuratibu masuala ya elimu, sayansi na teknolojia, pamoja na kukuza vipaji, ambapo pia alihimiza maendeleo zaidi ya kisayansi kufikiwa na kugeuzwa kuwa nguvu thabiti za uzalishaji.
Katika siku ya ufunguzi wa Mkutano wa Bunge (NPC), Waziri Mkuu Li Qiang aliwasilisha Ripoti ya Kazi ya Serikali ya 2025 kwa niaba ya Baraza la Serikali, ambayo inaweka bayana majukumu anuwai ya kiuchumi na maendeleo kwa ajili ya nchi kutekeleza katika mwaka huu mpya. Ripoti hiyo inajumuisha lengo la ukuaji wa Pato la Taifa la 2025 na inaelezea jinsi China inavyopanga kufikia malengo yake ya kiuchumi.
Baada ya kusikiliza ripoti hiyo kilichonivutia zaidi ni kuona namna watunga sera wanavyoweka mbele maisha ya watu. Ripoti hiyo imeeleza kwa kina jinsi serikali inavyoweka uwiano kati ya ukuaji wa uchumi na maendeleo ya kijamii, huku ikijaribu kukidhi matarajio ya watu wote kwa kuboresha maisha yao.
Ripoti ya kazi ya 2025, imetoa tathmini ya wazi juu ya vikwazo vinavyokabili uchumi wa China. Kwa upande wa kimataifa, ripoti imeonya kwamba mabadiliko ya kasi ya kimataifa na mazingira ya nje yanayozidi kuwa magumu yanaweza kuwa na athari kubwa katika sekta zake za biashara na teknolojia.
Mbali na hapo pia imebainisha kuwa matatizo ya ukuaji duni wa uchumi wa dunia, kuongezeka kwa hatua za upande mmoja na kujilinda kibiashara, na kuongezeka kwa vikwazo vya ushuru yanatatiza minyororo ya ugavi wa kimataifa na mzunguko wa kiuchumi. Halikadhalika kuongezeka kwa mvutano wa siasa za kijiografia kunapunguza zaidi matarajio ya soko na imani ya wawekezaji, na kuchangia kuongezeka kwa hali tete katika masoko ya kimataifa.
Katika vikao mbalimbali vya Mkutano wa Tatu wa Bunge la 14 la Umma la China, nilibahatika kuhudhuria kile cha mkoa wa Anhui. Ndani ya kikao wawakilishi wa nyanja mbalimbali kuanzia ya sayansi na teknolojia, utamaduni, wachumi na wengineo walikuwepo, ambapo kila mwakilishi alitoa tathmini ya utendaji wa mkoa huo kwenye sekta yake na baadaye kupata fursa ya kujibu maswali ya waandishi wa habari.
Wawakilishi wa Nyanja ya teknolojia walieleza hatua zilizopigwa na mkoa wa Anhui katika maendeleo ya teknolojia ikiwa ni pamoja na rikodi mpya iliyowekwa ya “Jua Bandia” la China katika kuelekea Uzalishaji wa Nishati Mchanganyiko.
Mikutano hii miwili ni muhimu sana, na ndio maana inafuatiliwa na nchi mbalimbali duniani, kwa kuwa athari yake sio tu inaonekana nchini China bali inaonekana hata katika nchi nyingine duniani. Moja ya kazi kubwa za mikutano hii miwili ni kutoa mwongozo wa mpango wa mwaka mzima wa maendeleo ya uchumi wa China, ikiwa ni pamoja na kuweka lengo la ukuaji wa uchumi na kutangaza sera za uchumi, ambapo mambo yote haya yanapatikana katika ripoti ya kazi ya serikali inayowakilishwa bungeni.
Mikutano Miwili mbali na kutunga sera za ndani ya nchi pia inatoa mwanga mkubwa juu ya sera ya nje ya China, ambapo kama destrui waziri wa mambo ya nje huwa na mkutano na waandishi wa habari kando ya mikutano hiyo.
Mwaka huu Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi, amekutana na wanahabari kutoka maeneo yote duniani na kujibu maswali yao tarehe 7 Machi. Waziri Wang aligusia masuala mbalimbali ya kikanda na kimataifa, kama vile Vita vya kibiashara na Marekani, mzozo wa Ukraine na mzozo wa Palestina na Israel pamoja na hali ya Gaza. Pia alifafanua sera za nje za China kuelekea Russia, Marekani, Ulaya na nchi za Dunia ya Kusini. Hivyo katika Mikutano Miwili ya mwaka huu, mapendekezo ya China kuhusu uhusiano wa kimataifa ni muhimu hasa kutokana na mabadiliko ya kasi na hali ya misukosuko ya kimataifa.
Wakati mwaka huu ni wa mwisho wa Mpango wake wa 14 wa Miaka Mitano (2021-2025), ni matumaini ya kila Mchina kwamba Mikutano hii itatoa fursa muhimu kwa China nchi ambayo ni ya pili kwa uchumi mkubwa duniani, kuharakisha mabadiliko yake kuelekea maendeleo ya hali ya juu na kuendeleza China ya kisasa.