Vikao vya Seneti vyaahirishwa hadi saa 11 baada ya Naibu Rais kuugua

Martin Mwanje
2 Min Read

Bunge la Seneti limeahirisha vikao vyake vya leo Alhamisi alasiri vya kusikiza mashtaka yaliyowasilishwa dhidi ya Naibu Rais Rigathi Gachagua. 

Vikao hivyo sasa vitarejelewa saa 11 jioni.

Hii ni baada ya Naibu Rais kubainika kuugua na kupelekwa hospitalini ili kupatiwa matibabu.

Hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa Naibu Rais anahudhuria vikao hivyo baada ya kupokea matibabu na yamkini kupata nafuu.

Ikiwa atapata afueni, Gachagua ambaye alikuwa katika Bunge la Seneti wakati wa vikao ya asubuhi, anatarajiwa kuanza kujitetea dhidi ya mashtaka 11 yaliyowasilishwa dhidi yake kwa lengo la kumtimua madarakani.

“Ukweli wa kuhuzunisha ni kwamba Naibu Rais ameugua. Huo ndio ukweli wa kuhuzunisha,” alisema Muite wakati akiitarifu Seneti kuwa mteja wake aliumwa.

Awali, kulikuwa na mashaka baada ya Naibu Rais kukosekana katika ukumbi wa Seneti wakati alipotakiwa kuanza kujitetea.

Gachagua alitarajiwa kuanza kujitetea majira ya saa 8:30 alasiri.

Hali hiyo ilimlazimu wakili mwandamizi Paul Muite kumuomba Spika Amason Kingi muda wa kwenda kubaini aliko mteja wake.

Subira subira hizo zilimfanya Seneta wa Kakamega Dkt. Boni Khalwale kumtaka Spika Kingi kuelezea mbona kanuni za bunge hilo zilikuwa zikikiukwa kufuatia kukosekana kwa Gachagua katika ukumbi wa bunge.

“Muda unayoyoma,” alilalama Dkt. Khalwale.

Hata hivyo, Spika Kingi alishikilia kuwa watamsubiri hadi Naibu Rais afikwe ukumbini kujitetea dhidi ya madai yake.

Spika Kingi alionya kuwa muda aliotengewa Naibu Rais hautaongezwa.

“Baada ya saa mbili, ikiwa Naibu Rais hatakuwa amefika ukumbini, nitatoa uamuzi wa kitakachofuata,” alisema Spika Kingi.

Wakati huo wote, Maseneta walitulia tuli kwenye viti vyao wakisubiri kuwasili kwa Naibu Rais anayekabiliwa na mashtaka 11 ya kufurushwa madarakani.

 

 

TAGGED:
Share This Article