Mabingwa wa Uropa – Paris saint Germain wamelazwa bao moja kwa nunge mapema hii leo na Botafogo (Brazil) katika mechi yao ya pili ya kipute cha klabu bingwa duniani kinachoendelea nchini Marekani. Bao hilo la pekee lilitingwa na mshambulizi matata Igor Jesus dakika za 36.
Katika uga wa Mercedes-Benz, kigogo Lionel Messi aliwaongoza Inter Miami kuwaadhibu Porto mabao mawili kwa moja.Magoli hayo yalipachikwa wavuni kupitia Telasco Segovia ( 47′) na nahodha Lionel Messi (54′) nalo la kuvitia machozi likifungwa na Samu Aghehowa (8′) (tuta).
Kwingineko, Atletico Madrid walivuna ushindi wa kwanza wa mabao matatu kwa moja dhidi ya Seattle Sounders. Matatu hayo yalitingwa na Pablo Barrios (11′ , 55′) na Axel Witsel ( 47′) huku lile la pekee likifungwa na Albert Rusnák ( 50′).
Mwisho ni mechi kati ya Pelmeiras na Ahly iliyoishia mabao mawili kwa nunge kwa faida ya Pelmeiras. Mabao hayo yalifungwa na Wessam Abou Ali ( aliyejifunga) ( 49′) na José Manuel López ( 59′ ).
Leo ijumaa ni zamu ya Benfica dhidi Auckland City saa moja jioni, Flamengo na Chelsea saa tatu, LAFC itakabana na ES Tunis saa saba usiku kisha Bayern wafunge na Boca Juniors saa kumi alfajiri.