Kenya na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, zimekubaliana kurejesha kikamilifu uhusiano wa kidiplomasia kufuatia mazungumzo kati ya Rais William Ruto na mwenzake wa DRC, Félix Tshisekedi, mjini Oyo, Jamhuri ya Congo.
Viongozi hao waliafikia makubaliano hayo katika Mkutano wa Ngazi za Juu wa Viongozi Wanne uliofanyika Novemba 22, 2026, kwa lengo la kupunguza mivutano na kuimarisha uhusiano wa nchi hizi mbili.
Katika taarifa kwenye mitandao ya kijamii, Rais Ruto alisema nchi hizo zimejitolea kufungua ukurasa mpya wa uhusiano wao unaotegemea kuaminiana, kuheshimiana na kushirikiana.
Miongoni mwa makubaliano hayo ni kurejesha uwakilishi wa kidiplomasia katika ngazi ya mabalozi, kuanzisha tena Tume ya Pamoja ya Ushirikiano na kuimarisha mashauriano ya mara kwa mara ya kidiplomasia.
Hata hivyo, nchi hizo bado zinatarajiwa kutekeleza hatua hizo ili kurejesha kikamilifu uhusiano wa kidiplomasia.
Viongozi hao pia wamekubaliana kuimarisha ushirikiano katika biashara, maendeleo ya kiuchumi, usalama na utamaduni, pamoja na kutumia njia za kidiplomasia kutatua mizozo.
Aidha, wamehimiza ushirikiano wa kikanda katika kukabiliana na janga la Ebola na kuimarisha juhudi za kulitokomeza.
Makubaliano hayo yalifikiwa kwa msaada wa Rais Denis Sassou N’Guesso wa Jamhuri ya Congo na mpatanishi wa Umoja wa Afrika, Rais wa Togo Faure Essozimna Gnassingbé.