Miili minne imepatikana baada ya mashua iliyokuwa imewabeba wahamiaji kupinduka katika pwani ya Senegal, huku shghuli za uokoaji zikiendelea.
Boubacar Seye, ambaye ni kiongozi wa kundi la Sans Frontieres, amethibitisha hayo, siku moja baada ya ajali ya mashua hiyo, ambapo awali mwili mmoja ulipatikana.
Afisa mmoja wa eneo hilo alisema takriban watu 50 walikuwa kwenye mashua hiyo ajali hiyo ilipotokea. Ajali hiyo inadaiwa ilitokea baada ya mashua hiyo kugonga mwamba.
Hadi kufikia sasa watu kadhaa bado hawajulikani walipo baada ya kutokea kwa ajali hiyo.
Ajali hiyo ilitokea huku visa vya watu kuvuka bahari kutoka magharibi mwa Afrika kuelekea bara ulaya vikiongezeka, huku mashua za wahamiaji hao zikizuiliwa au kuokolea kila siku.