Awamu ya 7 ya Filamu Creatives yaendelea Migori

Mpango huo unaendeshwa na Sanara Kenya na Filamujuani, Tume ya Filamu ya Kenya na Hazina ya Maendeleo ya Maeneo Bunge ya Uriri.

Marion Bosire
1 Min Read

Toleo la saba, la mpango wa mafunzo wa Filamu Creatives, limezinduliwa rasmi katika Kaunti ya Migori.

Watengenezaji filamu chipukizi wameanza mafunzo ya wiki nne yanayolenga utayarishaji wa sauti katika filamu.

Mafunzo hayo yanafanyika katika kituo cha uundaji filamu cha Uriri almaarufu ‘Uriri Film Hub’, huku somo la kwanza likitambulisha washiriki kwa matumizi ya sauti kwenye filamu, likijumuisha mazungumzo, sauti za mazingira, athari za sauti na muziki.

Mpango huo unaendeshwa na Sanara Kenya na wakfu wa Filamujuani kwa ushirikiano na Tume ya Filamu ya Kenya na Hazina ya Maendeleo ya Maeneo Bunge ya Uriri.

Washiriki watanufaika na mafunzo ya vitendo yanayofadhiliwa kikamilifu, yanayolenga kuwapa ujuzi wa kiufundi na maarifa ya ubunifu yatakayowawezesha kutumia fursa zilizopo katika tasnia ya filamu.

Wakfu wa Filamujuani ulianzishwa mwaka 2008 na Ken Oloo na Eva Wanjiku kwa lengo la kuwezesha vijana wasio na fursa za kutosha, wanawake, walemavu na wakimbizi kupitia mafunzo ya vitendo ya utengenezaji filamu.

Matoleo yaliyotangulia yamewapa washiriki mafunzo katika uandishi wa miswada, uongozaji, upigaji picha, utayarishaji wa sauti na uhariri.

Mpango huo pia umepanuka kutoka Nairobi hadi maeneo mengine, huku toleo la tano likihitimisha washiriki 117 Nakuru na la sita likikamilika Kisumu Julai 2026.

Share This Article