Shirika la ndege la Emirates limeanza kutumia ndege yake mpya ya Airbus A350 katika safari za kati ya Nairobi na Dubai.
Hatua hiyo inalenga kuongeza huduma za usafiri wa kiwango cha juu kwa abiria wanaosafiri kati ya Kenya na masoko ya kimataifa.
Ndege hiyo iliwasili kwa mara ya kwanza katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, JKIA leo Alhamisi, Novemba 12, 2026, na sasa itatumika katika safari za EK717 na EK718 kati ya Nairobi na Dubai.
Emirates sasa imeleta huduma ya Premium Economy nchini Kenya kwa mara ya kwanza, ikiwapa abiria chaguo la ziada kati ya daraja la Business na Economy.
Ndege ya A350 itachukua nafasi ya Boeing 777 katika safari hizo mbili za asubuhi. Hata hivyo, safari nyingine mbili za kila siku kati ya Nairobi na Dubai zitaendelea kutumia ndege za Boeing 777.
Makamu wa Rais wa Emirates anayesimamia shughuli za kibiashara katika eneo la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Rashid Al Ardha, alisema Kenya ni soko muhimu kwa shirika hilo kutokana na ongezeko la mahitaji ya usafiri wa anga na abiria wanaounganisha safari zao kupitia Dubai kuelekea Ulaya na Marekani.
Emirates ilianzisha safari ya tatu ya kila siku kati ya Dubai na Nairobi mwezi Julai na kuongeza safari zake katika JKIA hadi 21 kwa wiki.