Waisraeli wakumbuka mashambulizi ya Oktoba 7, miaka mitatu baadaye

KBC Digital News
2 Min Read
Picha kwa hisani ya EPA/Shutterstock

Israel leo inaadhimisha miaka mitatu tangu mashambulizi ya Hamas ya tarehe 7 Oktoba 2023, ambapo takribani watu 1,200 waliuawa na wengine 251 kutekwa nyara.

Israel ilijibu mashambulizi hayo, yaliyoelezwa kuwa mabaya zaidi dhidi ya Wayahudi tangu Vita vya Pili vya Dunia na mauaji ya Holocaust, kwa kuanzisha operesheni kubwa ya kijeshi katika Ukanda wa Gaza.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza inayosimamiwa na Hamas, zaidi ya Wapalestina 74,200 wameuawa katika vita hivyo.

Hamas na Israel zilifikia makubaliano ya kusitisha vita mwezi Oktoba mwaka jana chini ya mpango wa amani wa vipengele 20 uliopendekezwa na Rais wa Marekani, Donald Trump. Makubaliano hayo yalijumuisha kusitishwa kwa operesheni zote za kijeshi na kuachiliwa kwa mateka waliokuwa wamebaki mikononi mwa Hamas.

Hata hivyo, Wizara ya Afya ya Gaza inasema kuwa zaidi ya watu 1,460 wameuawa katika mashambulizi ya Israel tangu kusitishwa kwa mapigano kutangazwe. Kwa upande wake, jeshi la Israel linasema linaendelea kuwafuatilia makamanda wa Hamas na watu wanaowashutumu kuwa magaidi.

Matukio mbalimbali ya kumbukumbu yamepangwa kote nchini Israel kuwakumbuka waathirika wa mashambulizi ya 7 Oktoba. Miongoni mwa maeneo muhimu ya kumbukumbu ni eneo la tamasha la muziki la Nova, ambapo mamia ya watu waliuawa au kutekwa nyara wakati wa mashambulizi hayo.

Maadhimisho hayo yanafanyika huku athari za vita hivyo zikiendelea kuonekana kwa pande zote mbili, na huku juhudi za kidiplomasia za kudumisha usitishaji wa mapigano zikikabiliwa na changamoto mbalimbali katika ukanda huo.

Taarifa ya BBC

Share This Article