Mwanamuziki mkongwe wa mtindo wa kufoka foka almaarufu Hip Hop nchini Tanzania Joh Makini amezungumza kuhusu kutokuwepo kwenye tamasha ya BongoFleva@30 mjini Arusha ambapo ni nyumbani kwao.
Akizungumza kwenye mahojiano, Makini alielezea kwamba hakuhudhuria tamasha ya Jumamosi Septemba 19, 2026 mjini Arusha kwa sababu hakualikwa.
Msanii huyo alisema pia kwamba waandaaji wa tamasha hiyo, hawakualialika pia kundi lao la WEUSI.
Makini amesema alialikwa kushiriki Tamasha la ufunguzi wa Maadhimisho ya Miaka 30 ya Bongo Fleva iliyofanyika jijini Dar es salaam, lakini hakufanikiwa kuhudhuria.
Anaelezea kwamba wakati huo alikuwa nje ya Tanzania kwa shughuli za kibiashara na kimuziki.
Kwa upande mwingine, Joh Makini amesema hana tatizo na Msanii yeyote na kwamba katika umri aliofikia hatarajii kuwa na migogoro na Mtu, huku akisisitiza kuwa yuko tayari kufanya kazi na Msanii yeyote bila kujali tofauti zilizopo.
Joh Makini ambaye jina lake halisi ni John Simon Mseke ni mwanamuziki na Afisa Mkuu Mtendaji wa kamuni yake ya muziki iitwayo, Makini Music.
Mzaliwa huyo wa mkoa wa Arusha alianza muziki mwisho wa miaka ya 1990 katika kundi la River Camp lakini mwaka 2004 ndio alianza kupata umaarufu kutokana na kazi kama “Hawapendi” na “Hao”.
Mwaka 2006 ndio Joh Makini alijulikana kitaifa nchini Tanzania kufuatia wimbo wake uitwao “Chochote Popote”.