Bodi ya Hakimiliki ya Kenya, KECOBO, imewaalika wananchi kuwasilisha maoni yao kwa njia ya maandishi na kwa njia ya mazungumzo kuhusu utoaji leseni.
KECOBO inataka kupima ufaafu wa mashirika sita yanayotafuta leseni za kufanya kazi kama Mashirika ya Usimamizi wa Pamoja wa Hakimiliki, CMOs.
Tangazo hilo linafuatia jingine lililochapishwa Septemba 4, 2026, likialika waombaji kutuma maombi ya leseni za CMO.
Taasisi hiyo imesema wahusika wanaovutiwa wanaweza kutoa maoni kuhusu waombaji hao kwa mujibu wa Kanuni ya 11(2)(c) ya Kanuni za Hakimiliki (Usimamizi wa Pamoja), 2020.
Waombaji hao sita ni Music Copyright Society of Kenya, MCSK, Film Makers Rights Achievers of Kenya, FRAK, KAMP, Boralways Limited, Performing and Audio-Visual Rights Society of Kenya, PAVRISK na Collective Management Services Ltd.
Mashirika hayo yameomba kusimamia aina mbalimbali za hakimiliki, zikiwemo za kazi za muziki, kazi za sauti na picha, rekodi za sauti, haki za waandishi, wasanii, wachapishaji na haki nyingine zinazohusiana.
KECOBO pia itaendesha kikao cha hadhara Jumatatu, Oktoba 5, 2026, katika Ukumbi wa SHA kuanzia saa mbili unusu asubuhi hadi saa sita unusu mchana.
Maoni ya maandishi yanapaswa kuwasilishwa kufikia Jumatano, Oktoba 7, 2026, saa 11 jioni.
Leseni ambazo hutolewa na KECOBO ni za muda wa mwaka mmoja, na mashirika husika yanafaa kuomba kuhuishwa kwa leseni zao miezi mitatu kabla ya muda wa leseni kufikia kikomo.