Waziri wa Israel atishia kupokonya watengenezaji filamu uraia kisa filamu kuhusu Gaza

Filamu hiyo iitwayo NAZA ilishinda Tuzo Maalum ya Majaji katika Tamasha ya Filamu ya Venice.

Marion Bosire
2 Min Read
Rachel Szor na Yuval Abraham, waandaaji wa filamu ya NAZA

Waziri wa Utamaduni wa Israel, Miki Zohar, amesema atachukua hatua za kuwanyang’anya uraia watengenezaji filamu Yuval Abraham na Rachel Szor.

Hii ni baada ya filamu yao ya hali ya Israel katika Gaza, NAZA, kushinda Tuzo Maalum ya Majaji katika Tamasha ya Filamu ya Venice.

Katika ujumbe aliochapisha kwenye X Jumapili, Zohar aliita filamu hiyo chukizo na ushindi wake katika tamasha hiyo kuwa wa kushangaza.

Aliwatuhumu watengenezaji hao kwa kuidhuru nchi kwa ajili tu ya kupata makofi kutoka kwa wapinga Uyahudi kote duniani.

Waziri huyo alisema hatua za Abraham na Szor zinajumuisha usaliti dhidi ya taifa.

“Kwa kuwa mimi ni waziri wa utamaduni, nitachukua hatua mara moja kuwanyang’anya uraia wa Israel watengenezaji hao wanaochukiza kwa usaliti dhidi ya taifa,” aliandika.

Filamu hiyo ya dakika 80 inaeleza madai ya matumizi ya mifumo inayotumia akili unde na Israel kufanya mauaji ya halaiki yaliyopangwa dhidi ya Wapalestina huko Gaza, kwa mujibu wa muhtasari rasmi wa Tamasha la Filamu la Venice.

Filamu hiyo ilipokelewa kwa makofi ya dakika 25 baada ya kuonyeshwa kwa mara ya kwanza katika tamasha hiyo.

Inawashirikisha wanajeshi na maafisa wa ujasusi wa Israel waliotoa ushahidi kwa masharti ya kutotajwa majina.

Waliohojiwa walieleza kuhusu mfumo wa akili unde unaoitwa “Lavender”, unaodaiwa kutumika kufuatilia mawasiliano ya simu kati ya Wapalestina huko Gaza na kubaini watu wanaolengwa kuuawa.

Abraham alisema anatumai filamu hiyo itazishinikiza serikali za nchi za Magharibi kuweka vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Israel.

Share This Article