Namakula: Lafudhi ya kiingereza ni kikwazo kwa wasanii Uganda

Lafudhi hiyo alisema inaweza kufanya muziki wao usivutie sana au usieleweke kwa urahisi na wasikilizaji kutoka nchi nyingine.

Marion Bosire
1 Min Read
Rema Namakula, Mwanamuziki wa Uganda.

Mwanamuziki wa Uganda Rema Namakula ametoa maoni yake ya kweli kuhusu kwa nini ni vigumu kwa wanamuziki wa Uganda wanaoimba kwa Kiingereza kuingia katika soko la kimataifa.

Kwa mujibu wa Rema, changamoto moja kuu ni lafudhi au ukipenda jinsi wasanii wa Uganda wanavyotamka maneno ya kiingereza na kuzungumza Kiingereza.

Wakati mwingine lafudhi hiyo alisema inaweza kufanya muziki wao usivutie sana au usieleweke kwa urahisi na wasikilizaji kutoka nchi nyingine.

Kulingana na Rema, wasanii ambao wamesafiri sana na kuwasiliana na watu kutoka nchi mbalimbali wana uwezekano mkubwa wa kuelewa aina ya matamshi na uwasilishaji wa Kiingereza unaoweza kueleweka na hadhira ya kimataifa.

“Ikiwa umesoma au kusafiri katika mataifa mbalimbali ili kujifunza jinsi watu wanavyozungumza Kiingereza, basi Kiingereza hicho kinaweza kueleweka na watu wengine. Tunapozungumza au kuimba kwa lafudhi yetu wenyewe ya Kiingereza, hakivutii sana watu walio nje.” Alielezea.

Hata hivyo, Rema alionya wasanii wasijaribu kupita kiasi kuiga lafudhi za kigeni, akisema kufanya hivyo kunaweza kuwafanya waonekane sio wakweli au sio wa asili.

Alimtaja mwanamuziki mwenzake wa Uganda, Joshua Baraka, kama mfano wa msanii ambaye matamshi na namna yake ya kuwasilisha nyimbo vimemsaidia kuunganisha muziki wake na wasikilizaji nje ya Uganda.

Share This Article