Tamasha ya Kizimkazi awamu ya mwaka 2026 inatarajiwa kufanyika kuanzia kesho Agosti 12 hadi 14, katika uwanja wa Kizimkazi na Mwewe, Makunduchi, Kusini Unguja, kisiwani Zanzibar.
Tamasha hiyo itajikita katika utamaduni, utalii, michezo na uwekezaji, ikiwa na kaulimbiu “Kizimkazi Kumenoga!”
Tamasha hiyo itahusisha uzinduzi wa miradi ya maendeleo, maonyesho ya biashara, mipango ya kijamii na shughuli za michezo, ikiwemo mechi maalumu za mpira wa miguu kati ya Simba na Yanga.
Waandaaji pia wanalenga kutangaza utalii wa fukwe na pomboo, urithi wa Zanzibar pamoja na mipango ya maendeleo ya jamii.
Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa tamasha hiyo, huku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akitarajiwa kuhudhuria hafla ya kufunga.
Viongozi wa serikali, wawekezaji, wadau wa utalii na maelfu ya wananchi wanatarajiwa kushiriki katika tamasha hiyo ya siku tatu.
Programu za jioni zitajumuisha burudani za Taarab, Singeli, Bongo Flava na vichekesho, kutoka kwa wasanii kama Frida Amani, Alikiba, Nandy, Harmonize, Mbosso na Marioo, huku tamasha ikitoa fursa ya kuendeleza utamaduni, utalii, biashara na maendeleo ya jamii.
Tayari Makamu wa Rais wa Tanzania Emmanuel Nchimbi amewasili Zanzibar, leo Agosti 11, 2026, anakotarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika Ufunguzi wa Jengo la Dakhalia katika Skuli ya Sekondari ya Hasnuu Makame – Kibuteni Unguja.