Prisca Lyimo ambaye ni mshikilizi wa taji la Miss Grand Arusha mwaka huu wa 2026, ametangazwa kuwa Miss Cosmo Tanzania 2026 baada ya kuibuka mshindi wa pili katika fainali za mashindano ya Miss Grand Tanzania 2026.
Hafla hiyo ilifanyika jana katika ukumbi wa The Super Dome, ulioko Masaki, jijini Dar es Salaam.
Kupitia ushindi huo, Prisca atawakilisha Tanzania katika mashindano ya Miss Cosmo, moja ya majukwaa ya kimataifa yanayohamasisha dhana ya Urembo wenye mchango chanya kwa jamii, kwa kuwapa washiriki nafasi ya kuchochea mabadiliko chanya katika jamii kupitia miradi ya kijamii, uwezeshaji wa jamii na uhamasishaji kuhusu afya ya akili.
Prisca alikabidhiwa taji hilo na Jeska Michael, aliyekuwa Miss Cosmo Tanzania 2025.
Hafla hiyo pia ilitumika kuaga walimbwende wa vitengo mbali mbali washikilizi wa mataji ya mwaka 2025, tukio lililovutia hisia kali ukumbini Super Dome.
Walimbwende hao waliotwaa mataji mbalimbali mwaka 2025 walifanya tembezi la mwisho jukwaani almaarufu ‘Final Walk’, ikiwa ni ishara ya kuhitimisha rasmi kipindi chao cha utawala.
Walioaga jukwaa ni Beatrice Alex – Miss Grand Tanzania 2025, Amina Abdulkadri Jigge – Miss Earth Tanzania 2025, Jeska Michael Marwa – Miss Cosmo Tanzania 2025, Faidha Kassim Kivuyo – Miss Intercontinental Tanzania 2025, Efrazia Makene Mazigo – Miss Elite Tanzania 2025 na Jeniffer Augustine Shirima – Miss Africa International Tanzania 2025.