Chameleone aishukuru Tanzania

Aliangaziwa na kutuzwa kwenye awamu ya 4 ya Bongo Flava Honors iliyofanyika Julai 31, 2026 nchini Tanzania.

Marion Bosire
2 Min Read

Nguli wa muziki nchini Uganda Jose Chameleone ametoa shukrani za dhati kwa Tanzania kwa kumkubali na kumtuza kwenye Bongo Flava Honors.

Kupitia akaunti yake ya Instagram msanii huyo aliandika, “Mashabiki wangu, marafiki, na familia yangu, asanteni kwa kuendelea nami katika safari hii nzuri na ya kipekee”.

Aliendelea kuelezea kwamba heshima aliyoonyeshwa katika Bongo Flava Honors ni tukio ambalo atathamini na kukumbuka milele.

Msanii huyo alimtaja mamake mzazi aliyeandamana naye hadi Tanzania kushuhudia akituzwa akisema kwamba uwepo wake uliifanya siku hiyo kuwa wa kipekee zaidi.

Hakusahau waandaaji wa Bongo Flava Honors, vyombo vya habari na wanablogu kwa msaada wao na kwa kuendelea kutembea naye katika safari yake.

Jose Chameleone ndiye aliangaziwa na kutuzwa kwenye awamu ya 4 ya Bongo Flava Honors iliyofanyika Julai 31, 2026 nchini Tanzania, hafla iliyoanzishwa kwa lengo la kutambua waliotoa mchango mkubwa kwa muziki wa Tanzania maarufu kama Bongo Flava.

Akiwa jukwaani siku hiyo Chameleone alimshukuru Mungu kwa kumponya pamoja na mashabiki zake kwa kumwombea alipokuwa akiugua.

Wahusika wa tamasha hiyo huhitajika kutumbuiza moja kwa moja jukwaani pamoja na bendi.

Baada ya Tanzania, msanii huyo yuko nchini Kenya kwa ajili ya matamasha mbali mbali zikiwemo tamasha za wanamuziki Nameless na Redsan wanaosherehekea miaka 25 na 30 mtawalia katika tasnia ya muziki.

Share This Article