Mwanamitandao maarufu wa Tanzania Mwijaku amejipata katika hali ngumu baada yake kufungiwa nje ya boma yake kutokana na mzozo unaoendelea wa ardhi hiyo.
Akizungumza na wanahabari, mwanamitandao huyo ambaye jina lake halisi ni Burton Mwemba alielezea kwamba yeye na anaokaa nao walifukuzwa kwenye nyumba yake kutokana na hali hiyo huku ikizungushiwa utepe.
Kulingana naye, alinunua shamba husika kwa mzee fulani aliyemkabidhi hati kabisa kisha mwana wa mzee huyo akakwenda kuripoti polisi kwamba hatimiliki ya ardhi hiyo ilipotea akapatiwa nyingine na serikali.
Baadaye hati hiyo iliyotengenezwa ya pili, ilikabidhiwa kampuni fulani ya kuuza vipande vya ardhi ambayo tayari imeuza kipande hicho cha ardhi kwa mtu mwingine.
Kutokana na hilo, mwanamitandao huyo anashauri wanaotaka kununua ardhi, wahakikishe wananunua kwa watu wenye uwazi ambao watawapa hatimiliki halali na ambao hawana hila.
Mwijaku anakubali kwamba mchakato wa yeye kuuziwa kipande hicho cha ardhi haukuwa umenyooka na huenda akapoteza kila kitu ila ameanzisha utaratibu wa kuona iwapo atarejesha mali yake.
Kuhusu wanaomlaumu wakisema kwamba mdomo umemponza, Mwijaku alisema kwamba yeye kazi yake ni mdomo na amejikuta kwenye matatizo na ndiyo hali ya maisha changamoto hazikosi.