Mpango wa kutwaa silaha haramu washika kasi

NPS imekusanya jumla ya bunduki haramu 357 na risasi 2,342 baada ya silaha nyingine kukabidhiwa kwa hiari Elgeyo Marakwet

Marion Bosire
2 Min Read

Kampeni ya Kenya ya kukabiliana na umiliki wa silaha haramu inaendelea kushika kasi, huku silaha zaidi zikikabidhiwa kwa hiari katika kaunti za Elgeyo Marakwet na Tana River.

Hatua hii inazidi kuimarisha juhudi za kurejesha usalama katika maeneo yaliyokumbwa na uhalifu wa kutumia silaha.

Huduma ya taifa ya polisi imetangaza kuwa Kaunti ya Elgeyo Marakwet sasa imefanikiwa kukusanya jumla ya bunduki haramu 357 na risasi 2,342 baada ya silaha nyingine kukabidhiwa kwa hiari.

Katika Kaunti ya Tana River, wakazi pia walikabidhi bunduki mbili aina ya AK-47 zilizokuwa zikimilikiwa kinyume cha sheria pamoja na risasi kumi za milimita 7.62.

Maafisa wa usalama wanasema kila silaha inayoondolewa mikononi mwa raia hupunguza hatari ya uhalifu wa kutumia nguvu kama vile wizi wa mifugo, ujambazi wa kutumia silaha na mashambulizi ya kulipiza kisasi, hivyo kuchangia kuifanya jamii kuwa salama zaidi.

Huduma ya Taifa ya Polisi, NPS imewapongeza wananchi waliojitokeza kuunga mkono kampeni ya kuondoa silaha haramu kwa kuzisalimisha na kutoa taarifa muhimu kwa vyombo vya usalama.

Kwa mujibu wa polisi, ushirikiano huo unaoendelea kuimarika ni nguzo muhimu katika mapambano dhidi ya ukosefu wa usalama, ukionyesha kuwa amani ya kudumu hujengwa kupitia imani, uwajibikaji wa pamoja na kuheshimu sheria, badala ya kumiliki silaha haramu.

Share This Article