Kenya imedhamiria kuimarisha ushirikiano wake na Madagascar kwa manufaa ya raia wa nchi hizo mbili.
Hayo yamesemwa na Rais William Ruto ambaye alijumuika na raia wa nchi hiyo kuhudhuria maadhimisho ya miaka 66 tangu ijinyakulie uhuru.
Ruto yuko nchini Madagascar kwa ziara rasmi ya kiserikali na alihudhuria maadhimisho hayo yaliyoandaliwa katika Uwanja wa Barea jijini Antananarivo.
Kupitia ukurasa wa X, Rais amesema mataifa hayo mawili yanaunganishwa na historia ya kupinga ukoloni na bidii ya raia wake.
“Tunathamini urafiki wetu wa muda mrefu na Madagascar na tumejitolea kuimarisha ushirikiano huu kwa manufaa ya raia wa mataifa hayo,” alisema Rais Ruto.
“Leo, tunasherehekea uimara wa watu wake na hatua thabiti iliyopigwa katika kujenga taifa thabiti na lililostawi zaidi. Maadhimisho haya yanaheshimu siyo tu ushindi wa siku zilizopita uliopatikana kwa udi na uvumba, bali pia utafutaji endelevu wa ustawi na mustakabali bora kwa wote.”
Kiongozi huyo wa taifa anatarajiwa kushiriki meza ya mazungumzo na utawala wa Madagascar huku sekta za kilimo, biashara, safari za ndege na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) zikiangaziwa.
“Pamoja tutapanua biashara, uwekezaji, kuimarisha ushirikiano wa baharini, kuboresha uunganishaji na kubuni fursa katika Bahari ya Bindi kama lango la biashara, uvumbuzi na ufanisi wa pamoja,” aliongeza Rais Ruto.
Kwenye ziara hiyo, Ruto ameandamana na Mawaziri Lee Kinyanjui wa Biashara, William Kabogo wa ICT, na Mutahi Kagwe wa Kilimo na Ustawi wa Mifugo.
Ujumbe wa Kenya pia unatarajiwa kushiriki kongamano la kibiashara kati ya Kenya na Madagascar.