Mabingwa wa Uingereza Arsenal watashuka katika uwanja wa Puskas, Jumamosi usiku dhidi ya mabingwa wa Ufaransa,PSG katika fainali ya Ligi ya mabingwa Ulaya.
Arsenal wanawania kumaliza ukame wa miaka 55 wa kushinda Kombe la Ligi ya Mabingwa Ulaya ,na walifuzu kwa fainali ya mwaka huu bila kupoteza mechi wakifungwa magoli sita pekee.
Timu hizo zitakutana kwa mara ya sita katika kombe hilo ,PSG wakishinda mbili,Arsenal wakashinda moja na michuano miwili kumalizikia sare.
Mwaka jana PSG waliibandua Arsenal katika nusu fainali mabao 2-1.
Arsenal wanajivunia kurejea kwa mlinzi Jurrien Timber, ambaye ameuguza jeraha tangu mwezi Machi wakati PSG, wakimkaribisha beki Achraf Hakimi, ambaye pia amekuwa nje kwa muda.
Makocha wote wawili Luis Enrique wa PSG, atalenga kuhifadhi taji wakati Mikel Arteta, wa Arsenal, akilenga taji ya kwanza ya Ulaya.
The Gunners waliongoza hatua ya makundi wakishinda mechi zote nane, wakati PSG, ikimaliza ya nane na kuwalazimu kufuzu kupitia mchujo.
Katika mchujo wa kwanza PSG waliibandua Monaco jumla ya magoli 5-4, kabla ya kuwatema nje Chelsea mabao 8-2, katika awamu ya 16 bora.
PSG waliibwaga Liverpool magoli 4-2, katika robo fainali na hatimaye kuitimua Bayern Munich 6-5, kwenye nusu fainali .
Arsenal iliwakwatua Bayer Leverkusen 2-1, katika raundi ya 16 bora na kuwapiga laza Sporting Lisbon, kutoka Ureno, bao moja nunge katika kwota fainali.
The Gunners pia walipata ushindi wa 2-1, dhidi ya Atletico Madrid, katika nusu fainali.