Waziri wa Ulinzi Soipan Tuya, ametoa wito wa ushirikiano dhabiti wa kijeshi ili kukabiliana na hatari za ugaidi, itikadi kali na uhalifu wa kupangwa katika kanda ya Afrika Mashariki.
Akizungumza Ijumaa wakati wa kufunga mazoezi ya pamoja ya vikosi kutoka mataifa ya Afrika Mashariki almaarufu Ushirikiano Imara 2026 Jijini Nairobi, Tuya alionya kuwa ukosefu wa usalama katika kanda hiyo, huenda ukahujumu ukuaji wa uchumi na kudhoofisha taasisi muhimu zilizopo.
Kulingana na Tuya mazoezi hayo ya kijeshi yamekuwa jukwaa muhimu la kujifunza mikakati ya usalama, kuimarisha ushirikiano na kuratibu hatua za pamoja miongoni mwa mataifa washirika.
Zaidi ya wanajeshi, maafisa wa polisi na raia 400 kutoka mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walishiriki katika mazoezi hayo, huku Somalia ikishiriki kama mwangalizi.
Mazoezi hayo yaliwaleta pamoja maafisa wa usalama kutoka mataifa mbalimbali ya kanda hii kwa lengo la kuimarisha uwezo wa kukabiliana kwa pamoja na vitisho vinavyoibuka katika eneo hili.