Rais William Ruto ameahidi kujenga madarasa 30 mapya pamoja na maabara sita katika shule ya Njiiri, iliyo katika kaunti ya Murang’a.
Akizungumza alipozuru taasisi hiyo ya elimu, kiongozi wa nchi alisema kwamba serikali inasasisha na kupanua miundomsingi katika shule za sekondari ya juu kote nchini.
Kulingana naye, hatua hiyo inalenga kuhakikisha kwamba shughuli za masomo zinatekelezwa katika mazingira bora na salama.
Katika shule hiyo ya Njiiri, Rais aliongeza kusema kwamba wizara ya elimu itajenga jumba la afisi kwa gharama ya shilingi milioni 70 na idara ya nyumba ijenge bweni litakalotosha wanafunzi elfu moja.
Vile vile mamlaka ya barabara za mashambani imeelekezwa iweke lami katika njia zote za ndani za taasisi hiyo kurahisisha ufikiaji kwa wanafunzi na hata walimu.
Yote haya Rais alifafanua kwamba yanalenga kuhakikisha kwamba taasisi hiyo ya elimu inaafikia viwango vya kitaifa baada ya kupandishwa hadhi hivi maajuzi na kushughulikia idadi inayoongezeka ya wanafunzi.
“Kwa kupanua na kusasisha mazingira ya masomo, tunampa kila mwanafunzi fursa sawa kukua na kuafikia uwezo wao kamili,” alisema Rais Ruto.
Kabla ya kuzuru shule ya Njiiri, Rais Ruto alihudhuria ibada katika kanisa la A.I.C. Githumu, eneo bunge la Kandara, kaunti ya Murang’a akiwa ameandamana na viongozi kadhaa wa eneo hilo.