Iran kupitia vyombo vya habari vinavyohusishwa na serikali, imesema kwamba imepokea majibu kutoka Marekani kuhusu pendekezo lake la hivi karibuni la mpango wa amani.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran Esmaeil Baghaei, alisema majibu hayo, yaliyowasilishwa kupitia Pakistan, sasa yanatathminiwa, kulingana na shirika la habari la Tasnim.
Marekani bado haijathibitisha rasmi kwamba imeijibu Tehran, lakini Rais Donald Trump anaripotiwa kuambia shirika la habari la Kan la Israel Jumapili kwamba pendekezo hilo halikubaliki kwake.
Vyombo vya habari vya serikali ya Iran vilisema mpango wa amani wa vipengele 14 wa Tehran uliitaka Washington kuondoa majeshi yake karibu na mipaka ya Iran, kumaliza mzingiro wa majini kwenye bandari za Iran na kusitisha uhasama wote, yakiwemo mashambulizi ya Israel nchini Lebanon.
Pia uliitaka makubaliano kati ya nchi hizo mbili kufikiwa ndani ya siku 30.
Vyombo vya habari vya Iran viliongeza kuwa pendekezo hilo lilihimiza pande mbili zinazopigana kuzingatia “kumaliza vita” badala ya kuongeza muda wa kusitisha mapigano uliopo.
Baghaei, alinukuliwa akisema kwamba “kwa sasa hatuna mazungumzo ya nyuklia”, jambo ambalo ni hitaji muhimu kwa Washington.
Iran imekuwa ikikanusha mara kwa mara kuwa inatafuta silaha za nyuklia na inasema mpango wake ni kwa madhumuni ya amani pekee, ingawa ndiyo nchi pekee isiyo na silaha za nyuklia iliyoboreshha urani karibu na kiwango cha silaha.
Jumapili, Trump alitangaza kuwa Marekani itasaidia nchi zenye meli zilizokwama katika Mlango wa Hormuz.
“Kwa manufaa ya Iran, Mashariki ya Kati, na Marekani, tumewaambia nchi hizi kwamba tutaziongoza meli zao kutoka kwa njia hizi zilizozuiliwa kwa usalama, ili ziweze kuendelea na shughuli zao kwa uhuru na ufanisi,” alisema katika chapisho kwenye mitandao ya kijamii bila kubainisha nchi zipi.
Trump alisema mchakato huo, aliouita “Project Freedom”, utaanza leo Jumatatu, akiongeza kuwa ikiwa utaingiliwa, basi uingiliaji huo “utashughulikiwa kwa nguvu”.
Iran imepunguza kwa kiasi kikubwa usafiri kupitia mlango huo tangu vita vilipoanza Februari. Marekani pia imeweka mzingiro wa majini kwenye bandari za Iran.
Siku ya Jumamosi, Trump alithibitisha kwamba Washington ilikuwa imepokea pendekezo la hivi karibuni la amani kutoka Iran.
Katika ujumbe mfupi kwenye Truth Social, rais wa Marekani aliandika: “Hivi karibuni nitakuwa nikipitia mpango ambao Iran imetutumia, lakini siamini kwamba utakubalika kwani bado hawajalipa gharama kubwa ya kile walichofanya kwa ubinadamu na dunia kwa miaka 47 iliyopita.”