Msanii wa Uganda Anne Kansiime amesikitikia sekkta ya burudani nchini Uganda, akikosoa wadau wakuu pamoja na taasisi kwa kile anachosema ni kukosa kutambua kazi zake.
Akizungumza kwenye mahojiano mchekeshaji huyo mashuhuri alifichua kuwa licha ya mchango wake katika sekta hiyo, anahisi kupuuzwa kwa kiasi kikubwa, hata na vyombo vya udhibiti kama Tume ya Mawasiliano ya Uganda, UCC.
“Hata UCC haijawahi kunitambua kwa sababu wanapowasiliana na mimi mara nying huwa inaonekana kama mimi ndiye ninawahitaji wao,” alisema Kansiime.
Aliongeza kuwa hata anapoitwa kushiriki katika matukio au warsha, mazungumzo mara nyingi huzingatia zaidi muda wake utakaohitajika badala ya kuthamini mchango wake.
Kansiime pia alikosoa tuzo za ndani, akisema amechoshwa nazo kwa sababu, kwa mtazamo wake, hazina maana halisi wala thamani, akishangaa jinsi mtayarishaji wa maudhui anatuzwa bila kupatiwa chochote kitakachomsaidia kuboresha maudhui yake.
Alikosoa pia utamaduni wa kutoa kile alichokiita “medali za chuma tu” bila msaada wowote wa vitendo kwa wabunifu.
Kulingana naye, kumtambua mtu kama “bora zaidi” katika kundi fulani kunapaswa kwenda zaidi ya majina na kujumuisha faida zinazoweza kuboresha kazi na taaluma zao.
Kansiime amemwomba Rais Yoweri Kaguta Museveni kutambua mchango wake katika tasnia ya ucheshi na ubunifu akiwa bado hai na anafanya kazi.
Alitoa mfano wa Rais huyo akisema alianza kutawala Uganda mwaka 1986 mwaka aliozaliwa akisema yeye na chama tawala NRM wana umri sawa na hivyo muda wake na mchango wake vinastahili kutambuliwa.