Bingwa wa Jumuiya ya Madola katika mbio za mita 100 Ferdinand Omanyala ataongoza kikosi cha Kenya kwa mbio za Dunia za kupokezana kijiti kati ya tarehe 2 na 3 mwezi ujao mjini Gaberone Botswana.
Kikosi hicho kimechaguliwa kufuatia majaribio ya siku tatu yaliyokamilika Jumamosi katika uwanja wa Ulinzi Complex.
Kenya itashiriki katika fani za mita 100 kwa wanariadha wanne kupokezana kijiti wanaume,mita 100 kwa wanariadha wanne kupokezana kijiti jinsia mchanyato,mita 400 kwa wanariadha wanne kupokezana wanaume na wanawake na mita 400 kupokezana kwa jinsia mchanyato.
Omanyala atatimka mita 100 kwa wanariadha wanne, akishirikiana na Samuel Chege,Steve Odhiambo,Meshack Babu,Mark Otieno na Moses Wasike miongoni mwa wengine.
Timu ya wanawake ya mita 100 kwa wanariadha wanne inawajumuisha Eunice Kadogo,Millicent Ndoro na Diana Awako.
Mercy Okoth,Hellen Syombua ,Mercy Chebet watashirikiana na Brian Tinega,Kelvin Kiprotich na Kevin Kipkorir wakilenga kuboresha medali ya shaba waliyotwaa mwaka jana huko Guanzou,China.

