Huku Mataifa mengi duniani yakikumbwa na uhaba wa mafuta kutokana na vita vya ghuba, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa maafisa wa serikali kupunguza matumizi ya mafuta.
“Ndani ya serikali tuna matumizi makubwa ya mafuta, magari ni mengi, safari zetu ni nyingi niwaombe sana tuanze kupunguza matumizi ya mafuta, kwa kuanza na ofisini kwangu ninapotembea kuanzia sasa wote nitawaingiza kwenye kibasi” alisema Rais huyo.
Kulingana na Rais huyo, vita hivyo vimesababisha kupanda kwa bei ya mafuta na upungufu wa bidhaa hiyo muhimu.
Aidha amesema kutangazwa kusitishwa kwa vita hivyo na kufunguliwa kwa mlango bahari wa Hormuz ni jambo la faraja.
”Hii inatupa matumaini makubwa sana kama serikali na ile kuruhusu tu meli za awali za Ufaransa,za Japan…..kidogo nimeona bei ya mafuta imeshuka kidogo sasa hii inatupa matumaini.” Alisema Rais huyo.
Aidha amesema upandaji wa bei ya mafuta umekuwa ukienda sambamba na kupanda kwa bei za bidhaa, hivyo amewataka wananchi kuwa watulivu.