Halmashauri ya Kilimo na Chakula (AFA), imeanzisha msako wa kuwafurusha wafanyabiashara haramu wa Macadamia katika kaunti 14 hapa nchini.
Operesheni hiyo inalenga kuwakinga wakulima dhidi ya kuhadaiwa, kudumisha viwango vya ubora na kupunguza wizi wa zao hilo kutoka shambani kabla ya kukomaa, hayo ni kulingana na maafisa wa serikali.
Akizungumza baada ya kutekeleza operesheni iliyosababisha kukamatwa kwa mfanyabiashara ambaye hajasajiliwa katika eneo la Kiganjo, Gatundu Kusini kaunti ya Kiambu, Naibu Mkurugenzi wa AFA Patrick Kirimi, alisema watakaopatikana wakikiuka sheria watafunguliwa mashtaka ya kuvunja sheria za kilimo cha Macadamia.
Aliongeza kuwa operesheni hiyo itaendelea katika kaunti zote 14 ambapo Macadamia hukuzwa, kwa lengo kukabiliana na shughuli zinazokiuka sheria na kusababisha madhara kwa wakulima.
Huku akidokeza kuwa taifa hili lilipata shiligi bilioni 5 kutokana na mauzo ya Macadamia nje ya nchi, Kirimi alisema halmashauri hiyo inashirikiana na wadau kuhakikisha wakulima wanafaidika zaidi kutokana na kilimo chao.