Mkewe Khaby Lame aambulia patupu

Aliwasilisha ombi la talaka akidai nusu ya mali ya Lame lakini hakupata chochote kwani ilibainika kwamba Lame hamiliki chochote.

Marion Bosire
1 Min Read

Mke wa jamaa aliye na wafuasi wengi zaidi kwenye mtandao wa TikTok, Khaby Lame aitwaye Wendy Thembelihle Juel, anaripotiwa kuambulia patupu kuhusiana na mali ya Lame.

Juel aliwasilisha kesi mahakamani akitaka talaka kutoka Khaby akidai nusu ya mali ya nyota huyo wa TikTok lakini mahakama ikamfahamisha kwamba hilo haliwezekani kwa sababu Lame hamiliki chochote, huku ikiridhia ombi la talaka.

Inaripotiwa kwamba Lame hajasajili mali yake kwa jina lake bali amefanya hivyo kwa jina la babake mzazi.

Tukio hili linaashiria mabadiliko makubwa katika maisha ya Lame kwani uhusiano uliofuatiliwa pakubwa mitandaoni tangu ulipofichuliwa sasa umefikia kikomo.

Khaby Lame alitangazia umma kuhusu uchumba kati yake na Wendy mwisho wa mwaka 2020 kabla yao kufunga ndoa ya faragha baadaye.

Lame ambaye wazazi wake ni wa asili ya Senegal na ambaye alizaliwa nchini Italia anafahamika kwa video zake za vichekesho kuhusu njia rahisi za kufanya mambo ambapo hasemi lolote.

Mashabiki sugu wa wawili hao wamekuwa wakikisia kwamba uhusiano wao hauko sawa kufuatia kutoonekana pamoja kwenye video kwa miezi kadhaa.

Stakabadhi za mahakama zilizochapishwa na majukwaa kadhaa mitandaoni zinaonyesha kwamba Wendy alitaja tofauti zisizoweza kusuluhishwa kuwa sababu kuu ya kutaka talaka.

Share This Article