Waziri wa zamani apatikana na hatia ya kuiba mabati Uganda

Jaji Jane Kajuga aliamua kwamba mbunge huyo wa zamani wa Bududa alipokea na kuhifadhi mali ya serikali iliyogeuzwa kutoka kwenye mpango wa umma akijua.

Marion Bosire
2 Min Read

Mahakama ya kupambana na ufisadi nchini Uganda imemkuta na hatia aliyekuwa Waziri wa Nchi wa Masuala ya Karamoja, Agnes Nandutu, katika kesi inayohusisha mabati.

Kesi hiyo ilitokana na hatua yake kugeuza matumizi ya mabati 2,000 yaliyokuwa yamekusudiwa kutolewa kwa jamii zilizo hatarini huko Karamoja.

Jaji Jane Kajuga aliamua kuwa mbunge huyo wa zamani wa eneo la Bududa alipokea na kuhifadhi mali ya serikali iliyogeuzwa kutoka kwenye mpango wa umma akijua.

“Nimeridhika kuwa upande wa mashtaka uliwasilisha ushahidi unaothibitisha bila shaka yoyote kuwa Nandutu alipokea mabati 2,000 kutoka ghala la OPM huko Namanve,” Jaji Kajuga aliamua.

Aliongeza kwamba Mahakama ilibaini kuwa kati ya Juni na Julai 2022, Nandutu alihusika na mali ya serikali iliyojumuisha mabati 2,000 ya gauge 28 yaliyokuwa na alama “Afisi ya Waziri Mkuu”.

Mbunge huyo wa zamani ambaye alikuwa pia Waziri alirudishwa rumande katika Gereza la Luzira akisubiri hukumu yake kuhusiana na kashfa hiyo maarufu.

Mabati hayo yalikuwa sehemu ya mabati mengi yaliyopatikana kupitia bajeti ya nyongeza ya takribani Shilingi bilioni 39.94 kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Mpango huo wa afisi ya Waziri Mkuu, ulikuwa na lengo la kusaidia juhudi za kupokonya silaha na kuwezesha jamii katika eneo la Karamoja kwa kusambaza misaada kwa watu walio katika mazingira magumu.

Ushahidi uliowasilishwa mahakamani ulionyesha kuwa kati ya mabati 95,044 yaliyopatikana na kuhifadhiwa Namanve, ombi la mabati 10,000 liliwasilishwa kwa ajili ya uzinduzi wa rais katika Wilaya ya Moroto.

Hata hivyo, ni mabati 1,000 pekee yaliyotolewa rasmi, na mengine yakasalia kwenye ghala.

Share This Article