Tume ya kuchunguza matukio ya baada ya uchaguzi Tanzania yaongezewa muda

Inatarajiwa kuwasilisha ripoti yake kwa Rais Samia Suluhu Hassan Aprili 24, 2026.

Marion Bosire
2 Min Read
Jaji Mohamed Chande Othman, Mwenyekiti, tume ya kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Tanzania

Tume iliyoteuliwa na Rais wa Tanzania Samia Suluhu kuchunguza matukio ya baada ya uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba mwaka jana imeongezewa muda wa kutekeleza majukumu yake.

Mamlaka ya Uteuzi nchini humo, iliridhia maombi ya muda wa ziada kwa tume ya kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.

Tume hiyo chini ya uenyekiti wa Jaji Mohamed Chande Othman, ilianza kutekeleza majukumu yake Novemba 20, 2025, na ilikuwa inatarajiwa kukamilisha kazi ndani ya siku 90, lakini sasa imeongezea siku 21 hadi Aprili 24, 2026.

Kulingana na mamlaka hiyo ya uteuzi, sababu za kuongeza muda huo ni pamoja na kuiwezesha Tume kukamilisha uchambuzi wa ushahidi, taarifa na maoni yaliyopokelewa, kutoa fursa kwa wataalamu wa uchunguzi wa kisayansi kushughulikia baadhi ya vielelezo vipya vilivyowasilishwa.

Sababu nyingine ni kuiwezesha Tume kukamilisha maandalizi ya Ripoti itakayowasilishwa kwa Rais na kutoa fursa kwa Tume kuandaa tafsiri ya Ripoti hiyo.

Kufuatia nyongeza ya muda, wananchi waliendelea kujitokeza kwa wingi tofauti na matarajio na tume iliendelea kupokea ushahidi, taarifa na maoni zaidi.

Tume hiyo inaendelea kuwashukuru wananchi na wadau wote waliotoa ushirikiano wakati wa kufanya uchunguzi, wakiwemo wale waliofika mbele ya Tume kutoa ushahidi, taarifa na maoni, waliopiga simu na kutuma jumbe, waliotuma ushahidi, taarifa na maoni kwa maandishi na waliowasiliana na Tume kwa njia za mitandao ya kijamii.

Share This Article